2013-03-23 11:18:15

Katekesi ya kina kuhusu Mafuta Matakatifu


Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, hivi karibuni amewaongoza Mapadre katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu,: haya ni Mafuta ya Wakatekumeni, Krisma ya Wokovu na Mafuta ya Wagonjwa. Ibada ambayo kimsingi inaadhimishwa Alhamisi Kuu.

Hii pia ni fursa kwa Mapadre kurudia tena ahadi zao za utii kwa Askofu Mahalia pamoja na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati wanaposhiriki katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu waliokabidhiwa na Mama Kanisa katika maeneo yao. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Katoliki Dodoma.

Katika Ibada hii, Askofu Nyaisonga alibariki Mafuta ya Wagonjwa yatakayotumika kuanzia sasa kwa kuwataka waamini kufahamu na kuthamini Sakramenti ya Mpako Mtakatifu. Kwa Waamini wagonjwa ambao wako kufani, Sakramenti hii inapania kuwapatia neema ya pekee ili kuweza kukabiliana na magumu haya yanayoweza kutokana na ugonjwa, uzee au hatari ya kifo. Matunda ya neema ya Sakramenti hii ni kumwezesha mgonjwa kujiunga na mateso ya Kristo, kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe na kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Mwamini anajaliwa nguvu, amani, ujasiri ili kuvumilia Kikristo mateso ya ugonjwa au uzee. Ni Sakramenti inayompatia mwamini msamaha wa dhambi, ikiwa kama mgonjwa hakuweza kupata fursa ya kuungama dhambi zake. Sakramenti ya Mpako Mtakatifu inamrudishia mwamini afya, kama inafaa kwa wokovu wa kiroho. Ni Sakramenti inayomwandaa mwamini katika safari ya kuuendea uzima wa milele.

Askofu Nyaisonga pia alibariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu yanayotumiwa wakati wa Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Amewakumbusha Mapadre kwamba, wao ni wazee na viongozi wa Kanisa; wanashiriki kwa namna ya pekee katika kulitumikia Kanisa kwa kuadhimisha na kugawa Mafumbo ya Kanisa. Mapadre wakitenda kwa nafsi ya Kristo na kulitangaza Fumbo lake, huyaunganisha maombi ya waamini na sadaka ya Kristo na kwamba, huduma yao ya Kikuhani huchota nguvu kutoka katika Sadaka ya Kristo. Ni viongozi waliopewa dhamana ya Kibaba ndani ya Kanisa.

Askofu Nyaisonga anasema kwamba, kwa vile Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza katika maisha yao, kwa kuambatana na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Mapadre wawe kweli ni kielelezo cha maisha adili na utakatifu na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watu wanaowazunguka. Waamini nao wanapaswa kuwaheshimu, kuwathamini, kuwaombea Mapadre wao na kamwe wasiwe ni kikwazo na chanzo cha kuanguka kwao kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.