Utunzaji bora wa mazingira unapania kuenzi zawadi ya maisha!
Wakati wa kusimikwa kwake kama Askofu mkuu wa Jimbo la Roma, hapo tarehe 19 Machi
2013, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha tena kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili
ya: maskini: kiroho na kimwili; wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Lengo ni kupania kutokomeza mambo yote yanayoendelea kusababisha umaskini, njaa na
maradhi.
Hapa kuna
haja ya kujenga mshikamano wa dhati unaosimamiwa na kanuni auni. Ni tukio ambalo lilihudhuriwa
na wakuu wa nchi na wawakilishi wa Serikali zaidi ya 132, changamoto ni kuendelea
kusimamia haki jamii, amani na utunzaji bora wa mazingira.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican wakati Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda na ujumbe wake
walipotembelea Studio za Radio Vatican, Mheshimiwa Christopher Mvula, kaimu Balozi
wa Tanzania nchini Ujerumani na Mwakilishi wa Tanzania mjini Vatican anasema, ujumbe
uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto ya Kanisa kuendelea kushikamana
na maskini kwa kuwajali na kuwasaidia katika mahitaji yao msingi.
Anasema,
utunzaji bora wa mazingira ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoka
na madhara makubwa yanayosabanishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi sehemu mbali
mbali za dunia. Utunzaji bora wa mazingira unapania kuenzi zawadi ya maisha.