2013-03-22 08:56:13

Ujumbe kwa vijana wakati wa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi: Jengeni utamaduni wa upendo, amani na majadiliano ya kina!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Jumapili ya Matawi, ambayo kimsingi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo, anatarajia kuwepo Visiwani Zanzibar. RealAudioMP3

Lengo la hija hii ya kichungaji ni kusali pamoja na Wakristo wa Zanzibar ambao kwa siku za hivi karibuni, wametikiswa sana katika misingi ya imani na maisha yao, kiasi cha kutishia uhai wa Kanisa Visiwani Zanzibar.

Kardinali Pengo anasema, anakwenda Zanzibar pia kuwasilisha salam na matashi mema na matumaini kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, anayependa kuwahakikishia kwamba, yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maisha yao kama Wakristo.

Kardinali Pengo akizungumzia kuhusu vijana, amewakumbusha kwamba, wao ni tegemeo kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni, lakini jambo la msingi ni kuanzia sasa ni kuifahamu, kuiungama, kuiishi na kuisali, kwa maneno machache; vijana wanapaswa kuifahamu misingi ya imani yao kama inavyofafanuliwa vyema kwenye Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Hii ni imani kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Huu ndiyo urithi mkubwa ambao Baba Mtakatifu Francisko amewachangamotisha wazee kuwarithisha vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kardinali Pengo anawakumbusha vijana kwamba, "wasijirushe na malimwengu" wakasahau kwamba, kuna Fumbo la Kifo wanalotembea nalo katika maisha ya kila siku.

Jambo la msingi tangu sasa vijana wanapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema muda, nguvu, mali na karama mbali mbali walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Maisha ni zawadi kubwa wanayopaswa kuitunza!

Kardinali Pengo akitoa ujumbe wake kwa vijana sehemu mbali mbali za Tanzania na Afrika kwa ujumla, anawahimiza vijana kutambua kwamba, si kwa nguvu na uwezo wao wa kibinadamu wataweza kulijenga Kanisa wala kuleta amani, utulivu na upatanisho katika Jamii, bali ni kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka, imani inayomwilishwa katika matendo, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa amani, majadiliano, upendo na mshikamano miongoni mwa watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.