Mchakato wa Katiba nchini Tanzania unaendelea kwa kasi nzuri, lengo ni kuwa na Katiba
Mpya ifikapo mwaka 2015
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha
kwamba, uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya
unalenga kuwapatia watanzania Katiba Mpya itakatokuwa ni dira na mwongozo kwa miaka
mingine hamsini ijayo.
Kwa sasa Tume
ya kurekebisha Katiba imemaliza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi katika maeneo
yote nchini Tanzania. Tume inafanya majumuisho na uchambuzi na hatua inayofuata ni
uandikaji wa Rasimu ya Katiba Mpya. Serikali imeanza kuunda Mabaraza ya Katiba kuanzia
vijijini hadi Baraza kuu la Taifa, ili kutoa fursa kwa wananchi kurutubisha na kuboresha
Rasimu ya Katiba Mpya. Rasimu ikishapitishwa na Baraza kuu la Taifa, itarudishwa tena
kwa wananchi ili waweze kuipigia kura ya maoni.
Waziri mkuu Mizengo Pinda
akiwa kwenye Studio za Radio Vatican amesema kwamba, hatua ambayo Tanzania imefikia
kwa sasa katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya inatia matumaini ya kuweza kuwa na
Katiba Mpya katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2015.