Alhamisi kuu, Papa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Gereza la watoto wadogo!
Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Alhamisi kuu hapo tarehe 28 Machi
2013, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya siku ile iliyotangulia kuteswa kwake Kristo,
alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu la Upadre, Sakramenti zinazofumbatwa
katika huduma kwa Mungu na jirani; jioni saa 11:30 saa za Ulaya, ataadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwenye Gereza la Watoto hapa mjini Roma.
Itakumbukwa kwamba,
Ibada ya Misa Takatifu Alhamisi kuu jioni, inakazia kwa namna ya pekee huduma ya upendo,
inayojionesha kwa Kristo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu, changamoto ya kuendeleza
huduma hii, kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu
Francisko katika utumishi wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, alizoea
kuadhimisha Ibada ya Alhamisi kuu, Hospitalini au Gerezani, kama kielelezo cha huduma
ya upendo wa Kristo kwa wale wanaojisikia kuwa wanyonge mbele ya macho ya walimwengu.
Baba Mtakatifu Francisko anapenda pia hata katika dhamana yake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro, kuendeleza utume huu miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Ibada za Juma kuu hapa mjini Vatican zitaendelea kadiri ya utaratibu
kutoka kwa Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa.
Itakumbukwa kwamba, Baba
Mtakatifu Benedikto XVI alitembelea Gereza la Watoto Wadogo, "Casal del Marmo" tarehe
18 Machi 2007 na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu katika Kikanisa cha Baba Mwenyehuruma
kilichoko kwenye taasisi hiyo.