2013-03-20 14:14:25

Ujumbe wa Tanzania mjini Vatican: mshikamano na wanyonge!


Waziri mkuu Mizengo Pinda, Mheshimiwa Christopher Mvula, kaimu balozi wa Tanzania nchini Ujerumani na mwakilishi wa Tanzania mjini Vatican pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania, Jumatano, tarehe 20 Machi 2013 walitembelea Radio Vatican, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Kanisa kuu la Yohane wa Laterano, Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta pamoja na maeneo mbali mbali ya kihistoria hapa mjini Roma. RealAudioMP3

Waziri mkuu Pinda pamoja na ujumbe wake, walikuwa mjini Roma kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Waziri mkuu alikuwa anamwakilisha Rasi Jakaya Kikwete na watanzania kwa ujumla.

Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha Makardinali kumchagua Papa Francisko ili kuliongoza Kanisa na kwa kupitia kwake, atasaidia pia mchakato wa kuimarisha utangamano wa nchi na dunia kwa ujumla. Ni kiongozi ambaye ametoa changamoto ya kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waweze kuondokana na baa la umaskini. Anawaalika watanzania na watu wenye mapenzi mema kushikamana na kuendelea kumwombea Papa Francisko ili aweze kufanikisha utume wake.

Akizungumzia kuhusu vurugu na mauaji ya viongozi wa kidini, matukio ambayo yameitikisa Tanzania kwa siku za hivi karibuni, Waziri Mkuu Pinda anasema kwamba, Serikali imechukua hatua za kisheria kwa kufanya uchunguzi wa kina kwa kila eneo na baadhi ya wahusika kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, lakini juhudi kubwa bado zinaendelea kuwasaka wahusika wa mauaji ya Padre Evarist Mushi aliyeuwawa Visiwani Zanzibar.

Waziri mkuu Pinda amesema kwamba, tarehe 4 Aprili 2013, Serikali pamoja na wadau mbali mbali watakutana kujadili mustakabali wa Tanzania, kwa kuangalia amani na utulivu kama nyenzo muhimu katika ustawi na maendeleo ya Tanzania. Ametumia fursa hii pia kuipongeza Radio Vatican kwa kazi kubwa inayofanya.









All the contents on this site are copyrighted ©.