Maskini hata katika umaskini wao wanaweza kuchangia kwa hali na mali kulistawisha
Kanisa
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar, SECAM, katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, kwake binafsi
anaona kwamba, kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu Francisko kuliongoza Kanisa Katoliki
ni paji la Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Ulimwengu mamboleo na kwa namna ya pekee kwa
Kanisa Barani Afrika.
Katika ulimwengu
mamboleo watu wamefikia hatua ya kudhani kwamba, kwa nguvu ya fedha, mali na uchumi
wanaweza kufanya jambo lolote hapa duniani. Baba Mtakatifu Francisko ni baraka kwa
Kanisa, hali inayojionesha hata katika uchaguzi wa jina lenyewe. Ni Mtakatifu aliyezaliwa
na kulelewa katika familia iliyobahatika kuwa na utajiri mkubwa.
Baada ya
kuongoka akaacha yote na kujitosa pamoja na wenzake kumjengea Kristo Kanisa. Mwanzoni
alidhani ni Kanisa la mawe, lakini pole pole alitambua kwamba, Kanisa alilokuwa anapewa
changamoto ya kulijenga ni Fumbo la Mwili wa Kristo, kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yanayojikita katika ufukara kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
Kardinali
Pengo anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ana njia zake na kamwe hawezi kufungwa na
fikara na mawazo ya binadamu. Uamuzi wa Francisko ulikuwa ni mzito, kiasi kwamba,
baba yake mzazi aliamua kufukuza kutoka nyumbani kwake.
Francisko akapewa changamoto
ya kulijenga Kanisa la Kristo lililokuwa limeanza kumezwa na malimwengu,kwa kutaka
mambo ya ufahari na mali, katika ulimwengu wa wakati ule! Watu walipima mafanikio
kwa wingi wa mali na madaraka aliyokuwa nayo mtu, wakasahau kwamba, madaraka ni kwa
ajili ya kuwahudumia wanyonge na maskini na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chimbuko
la mafanikio ya binadamu.
Kardinali Polycarp Pengo anasema, Baba Mtakatifu
Francisko alikwisha kuona na kuonja hadha ya umaskini na mahangaiko ya watu wa Argentina.
Akatambua kwamba, hawa ndio tegemeo la Kanisa. Akajitosa bila ya kujibakiza hata kidogo,
akasimama kidete kulinda na kuwatetea maskini, ambayo kwa uhuru kamili amethubutu
wawepo kwenye Ibada ya Misa Takatifu alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko hata baada ya kuchaguliwa kwake,
maneno yake ya kwanza kwanza yanayonesha changamoto kwa Kanisa katika kuwahudumia
maskini na kwamba, uongozi hauna budi kuwa ni huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Ni changamoto ambayo imeendelea kusikika hata katika Mahubiri
yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Siku ya Jumanne,
tarehe 19 Machi 2013.
Kardinali Polycarp Pengo anasema, Waamini Barani Afrika
hata katika umaskini wao, wanaweza kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo
ya Kanisa Barani Afrika. Hakuna sababu ya kukata tamaa na kwamba, umaskini au ufukara
wa Kiinjili si jambo linaloweza kuwa ni kikwazo cha kuchangia maendeleo ya Kanisa
Barani Afrika.
Hii ni changamoto kwa waamini Barani Afrika kushikamana na
kujifunga kibwebwe kutumia karama na vipaji walivyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa
ajili ya maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa ujumla wake. Wawe tayari kumsikiliza Mwenyezi
Mungu anayezungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu na kamwe kisiwepo
kisingizio tena!
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM anahitimisha mahojiano haya maalum na
Radio Vatican kwa kutolea ushuhuda jinsi ambavyo hata Makardinali walivyopigwa na
butwaa walipomwona Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kushirikiana nao kwa sala,
chakula na maongezi kama ndugu bila ya kujitenga, changamoto kubwa kwa sasa ni kumsikiliza,
kuona na kutenda kadiri ya maongozi yake!