2013-03-19 11:37:17

Papa Francisko na Bartolomeo wa kwanza wakumbatiana; changamoto ya kusonga mbele katika majadiliano ya kiekumene!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo amefuatilia kwa njia ya Luninga, Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Itakumbukukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, yuko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, tangu alipoamua kwa utashi na uhuru kamili kung'atuka kutoka madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa tangu ulipotokea Mpasuko wa Kanisa kunako mwaka 1054, takribani miaka elfu moja iliyopita, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli amehudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapoanza utume wake rasmi. Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wamekutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wanapeana busu la amani, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Papa Francisko.

Patriaki Bartolomeo amenukuliwa akisema kwamba, Makanisa haya mawili kadiri ya siku zinazovidi kusonga mbele yanazidi kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayopania kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo. Majadiliano kati ya Makanisa haya mawili yanajikita katika taalimungu na dhamana na nafasi ya Papa katika maisha na utume wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.