2013-03-19 09:20:55

Papa Francisko amtuma Kardinali Pengo kuwaimarisha ndugu zake katika imani Visiwani Zanzibar


Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hivi karibuni alipokutana na Baba Mtakatifu Francisko, alimtuma kwenda Zanzibar ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani. RealAudioMP3

Kutokana na agizo hili, Kardinali Polycarp Pengo, anatarajiwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, kushiriki na waamini wa Jimbo Katoliki Zanzibar kwa Ibada inayoliingiza Kanisa katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Kardinali Polycarp Pengo anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, ili Mwenyezi Mungu aweze kumlinda na kumwiimarisha katika utekelezaji wa malengo yake ya kitume. Papa Francisko akiishaimarika katika imani, matumaini na mapendo, aweze pia kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo, hasa wale wanaoishi katika wasi wasi na hofu ya madhulumu ya kidini. Wasikie na kuonja uwepo na sala za Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya maisha yao hapa duniani, kamwe wasidhani kwamba, wamesahaulika!







All the contents on this site are copyrighted ©.