Papa Francisko aanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu wa
Roma
Baba Mtakatifu Francisko ameanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati
huu Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu na mchumba
safi wa Bikira Maria. Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko anakuwa
pia ni Askofu wa Jimbo la Roma, Kanisa ambalo ni kielelezo cha upendo na mshikamano
na Makanisa mengine yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia.
Ibada ya kuanza
kwa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Francisko imesheheni utajiri mkuu wa mafumbo ya
imani.
Ibada ya Fumbo la Ekaristi Takatifu imeadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro, mahali ambapo kadiri ya Mapokeo, Mtakatifu Petro aliyamimina
maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro na viunga vya mji wa Vatican, vimesheheni watu kutoka sehemu mbali mbali za
dunia, waliofika mjini Vatican kushuhudia tukio hili la kihistoria. Takwimu zinazonesha
kwamba, zaidi ya viongozi wakuu wa nchi 132 wamehudhuria. Kuna wawakilishi wa dini
na madhehebu mbali mbali waliofika pia kuonesha moyo wa upendo na mshikamano katika
kumhudia mwanadamu katika hija ya maisha yake ya kiroho hapa duniani.
Baba
Mtakatifu Francisko ameanza tukio hili kwa kuzunguka na kuwasalimia waamini, mahujaji
na watalii waliofika kumshuhudia akianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro
na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Baadaye, Baba Mtakatifu alirudi kwenye Sakristia
ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa
Takatifu. Alipokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, alishuka kwenye
gari lake na kuenda kumsalimia mgonjwa aliyekuwa amebebwa na ndugu zake, waliokuwa
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu pamoja na wahusika
na wawakilishi walishuka kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, chini ya Altare kuu ya
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, akapata muda wa kusali na kutafakari
kidogo, wakati huo, tarumbeta zilikuwa zinapigwa kuonesha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu
Petro ameanza hija ya utume wake rasmi. Baba Mtakatifu amevikwa Palio takatifu, Pete
ya Ukulu wa Mtakatifu Petro ambayo si ya dhahabu na Injili ambayo ilikuwa imewekwa
kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, usiku uliokuwa umetangulia.
Baadaye, Baba
Mtakatifu pamoja na Makardinali na Maaskofu wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki walipanda
kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakati wote huo, Waamini walikuwa wanaimba
wimbo wa kumsifu Kristo Mfalme, wakitumia baadhi ya maneno yalitolewa kwenye Mtagsuo
Mkuu wa Pili wa Vatican. Litania ya Watakatifu iliimbwa.
Baba Mtakatifu ameadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu alisaidiwa na wakuu wawili wa Mashirika ya Kitawa: Mheshimiwa
Padre Josè Rodriguez Carballo, Mkuu wa Shirika la Wafranciskani pamoja na Padre Adolfo
Nicolas Pachon, Mkuu wa Shirika la Wayesuit. Kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba
Mtakatifu alivishwa Palio takatifu na Kardinali, shemasi Tauran, baadaye alivishwa
Pete ya Mvuvi na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali. Baadhi ya Makardinali
waliwawakilisha Makardinali wenzao kuonesha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.