Baba Mtakatifu Francisko ni tumaini la maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii!
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania, Manos Unidas ambalo limekuwa mstari
wa mbele katika kuonesha ushuhuda wa imani katika matendo kwa kuwahudumia maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali zao za maisha, linasema
kwamba, lina matumaini makubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume
wake, kwani ameonesha tangu awali wa mapambazuko ya utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wahitaji zaidi.
Manos Unidas
linachukua fursa hii kutoa mwaliko kwa Mashirika pamoja na Jumuiya ya Kimataifa, kuendelea
kulivalia njuga tatizo la umaskini, magonjwa na ujinga, ili dunia iweze kuwa ni mahali
pazuri zaidi pa kuishi. Kila mtu akitekeleza dhamana na majukumu yake, inawezekana
kabisa Jumuiya ya Kimataifa kupunguza hali ya umaskini wa hali na kipato mintarafu
Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015.
Changamoto hii ambayo
kwa wengi inaonekana kuwa ndoto inawezeka kufikiwa, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa
itaendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni miongoni mwa watu, daima
wakitafuta mafao ya wengi, haki, amani, udugu na mshikamano wa kimataifa. Hizi ni
kati ya fadhila ambazo zinapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko anapoanza
utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.