2013-03-18 11:12:44

Rais Robert Mugabe, kuhudhuria sherehe ya Papa Francis anapoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro


Wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza kuwasili mjini Vatican kwa ajili ya kushuhudia Baba Mtakatifu Francis akianza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu. Katika hotuba zake ambazo zinaonesha dira na mwelekeo wa maisha na utume wake, anaendelea kukazia umuhimu wa waamini kutembea katika mwanga wa Kristo, wakijenga na kuliimarisha Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Anasema kwamba, Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Kati ya viongozi mashuhuri kutoka Barani Afrika ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye kwa kawaida matukio kama haya yanayogusa masuala ya imani hakosekani kamwe. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2011 wakati Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipokuwa anamtangaza Yohane Paulo wa Pili kuwa Mwenyeheri alifika bila wasi wasi wowote, akisema kwamba, alikuwa na ibada ya pekee kabisa kwa Papa Yohane Paulo wa Pili.

Wakati wa maziko ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, kunako mwaka 2005 alitinga mjini Vatican licha ya kuwekewa vikwazo na Jumuiya ya Ulaya. Kunako mwaka 2008 Rais Mugabe alihudhuria pia mkutano wa FAO uliokuwa unafanyika mjini Roma.

Baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali waliokwishawasili ni pamoja na Rais Cristina Fernandez Kirchner wa Argentina na Rais Sebastian Pinera kutoka Chile. Watu wengine mashuhuri ni Bwana Perez Esquivel mshindi wa tuzo ya amani kutoka Argentina anasisitiza kwamba, Kardinali Bergoglio enzi ya utumishi wake nchini Argentina, hakuwahi kuunga mkono utawala wa mabavu nchini humo.

Marais wengine waliowasili tayari ni Taur Matan Ruan kutoka Timor ya Mashariki.







All the contents on this site are copyrighted ©.