2013-03-16 10:23:07

Viongozi wa Makanisa Zambia wanasema, wanayaona na kusikia kilio cha watu wao!


Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu… nimesikia kilio chao! Ni kauli mbiu ya ujumbe kutoka Umoja wa Makanisa ya Kikristo nchini Zambia, unaounganisha: Baraza la Makanisa Zambia, Baraza la Makanisa ya Kipententoste Zambia pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia. Viongozi hawa wa kidini wanasema, wameyaona madhulumu yanayoendelea nchini Zambia katika medani za kisiasa.
Kuna saratani ya rushwa na ufisadi, ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana; ongezeko kubwa la pengo kati ya maskini na matajiri; huduma duni za elimu, afya pamoja na ukosefu wa utawala wa sheria. Kuna uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu, changamoto kwa wananchi wa Zambia kuchunguza dhamiri zao, ili kuweza kuwarudishia watu matumaini yanayoendelea kupotea siku hadi siku!
Wananchi wameendelea kupoteza maisha katika kamepni za chaguzi ndogo nchini Zambia, jambo ambalo haliwezi kukubalika na kuliacha liendelee kutendeka miongoni mwa wananchi wa Zambia, kiasi cha kuhatarisha amani, utulivu na demokrasia ambayo wameitafuta kwa udi na uvumba. Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa utawala bora; haki, amani, utulivu na demokrasia inayozingatia ukweli na uwazi.
Viongozi wa Makanisa wanasikitika kusema kwamba, chaguzi ndogo ambazo zimeendelea kufanyika nchini Zambia, hata kama ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba ambayo ni Sheria Mama, zimeonesha mapungufu makubwa, kiasi kwamba, zinatumiwa na baadhi ya viongozi kuonesha uchu wa mali na madaraka na kwamba, matukio yote haya si bure, lazima kuna mkono wa mtu! Hizi ni changuzi ambazo zinaendelea kutumia kiasi kikubwa cha fedha ambazo kimsingi zilipaswa kutumika katika maboresho ya sekta ya elimu na afya kwa ajili ya wananchi wengi wa Zambia.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Serikali ya Zambia imepoteza mwelekeo wa vipaumbele katika maisha ya wananchi wake. Ni matumaini ya viongozi wa Kanisa kwamba, muswada wa Katiba Mpya ya Zambia, utarekebisha mapungufu yanayoendelea kujionesha katika changuzi ndogo nchini humo, ili kweli ziwe ni kwa ajili ya mafao na ustawi wa demokrasia ya kweli.
Viongozi wa Makanisa katika tamko lao la pamoja, wanaiomba Serikali kutumia madaraka yake kikamilifu kwa ajili ya kuwaongoza wananchi wa Zambia, kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na utulivu, daima wakitafuta mafao ya wengi sanjari na kujenga majadiliano yanayopania ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia. Serikali kamwe isitumie nguvu kupita kiasi, bali itoe kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya wananchi wa Zambia kwa kuwapatia vijana fursa za ajira, huduma na mahitaji msingi.
Viongozi wa Makanisa wanawaalika wanasiasa kwa namna ya pekee, kuondokana na ubinafsi, ukabila, vitisho, chuki na uhasama na badala yake waoneshe ukomavu, utu n aari ya kutaka kuwaongoza wananchi wa Zambia kwa unyofu, wakikumbuka kwamba, cheo ni dhamana. Wanasiasa wajikite kutafuta mafao ya wengi, badala ya kujitafuta wenyewe. Ikiwa kama wanasiasa wataendekeza siasa za chuki na uhasama, demokrasia nchini Zambia itachechemea hatimaye, kudhoofu kabisa.
Jeshi la Polisi, wanasema viongozi wa Makanisa linawajibu wa kulinda na kutekeleza sheria za nchi. Kuna shutuma kutoka kwa wananchi kwamba, Jeshi la Polisi limekuwa likitumiwa na baadhi ya ”vigogo” Serikalini kwa ajili ya mafao yao binafsi, hali inayojenga picha potofu ya Jeshi la Polisi nchini Zambia. Viongozi wa Makanisa wanalitaka Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia utawala wa sheria, haki, weledi na sera za nchi. Wasikubali kutumiwa na viongozi wa kisiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Vyombo vya Upashanaji Habari vimeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa wananchi wa Zambia, lakini vyombo hivi pia vinaanza kupoteza sifa, maadili na kanuni zinazoongoza vyombo hivi vinavyopaswa kutafuta na kutangaza ukweli. Vyombo vya habari visitumike kwa ajili ya kuwachafua baadhi ya viongozi kwa kujenga chuki na uhasama, mambo ambayo hayana tija kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Zambia!
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawishaji wa demokrasia kwa kutumia mikakati mbali mbali na elimu ya umma. Mashirika haya yanachangamotishwa kuheshimu uhuru wa wananchi wakati wa mchakato wa kupiga kura.
Viongozi wa Makanisa wanawataka kwa namna ya pekee kabisa wale waliopewa dhamana ya kuwaongoza Wazambia katika maisha ya kiroho kuachana kabisa kushabikia masuala ya kisiasa, bali wasimame kidete, kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; ukweli, uhuru, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; msamaha na upatanisho wa kitaifa!
Ni wajibu kwa wananchi wa Zambia kuachana kabisa na tabia ya kujihusisha na vurugu na fujo zinazopelekea watu kupoteza maisha na mali zao. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha utamaduni wa umoja wa kitaifa; uaminifu, utu na maadili mema; ukweli, uwazi na uwajibikaji; arin a moyo wa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa; kupenda na kusamahe. Ni mwaliko wa kudumisha demokrasia, uhuru na utawala bora. Kila raia awajibike katika kutumia vyema uhuru wake wa kujieleza kwa ajili ya mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.