2013-03-16 09:08:12

Vijana wako tayari kumpokea Papa Francis wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, 2013


Askofu mkuu Joao Orani Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro, Brazil, mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa yatakayoanza kutimia vumbi kuanzia tarehe 23 hadi 28 Julai, 2013 mjini Rio de Janeiro. Waamini na kwa namna ya pekee vijana, wamepokea taarifa ya kuchaguliwa kwa Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa mikono miwili. Wanatambua kwamba, kwa hakika wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 watakuwa na Baba, Mwalimu na Mtumishi wa watumishi wa Mungu.

Kanisa tayari limekwisha jipanga kumpokea na kumkirimia Khalifa wa Mtakatifu Petro atakapokwenda nchini Brazil kukutana na kuwaimarisha vijana katika hija yao ya kujenga na kuimarisha Kanisa, daima wakiwa makini katika kumtolea ushuhuda Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu!

Askofu mkuu Tempesta anasema, Kanisa la Amerika ya Kusini, linatambua na kuthamini mchango wa Baba Mtakatifu Francis wakati wa utume wake alipokuwa nchini Argentina. Kanisa, lakini vijana kwa namna ya pekee, wako tayari na makini kumpokea Baba Mtakatifu Francis, wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25, tangu Siku ya Vijana Duniani ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza Amerika ya Kusini.








All the contents on this site are copyrighted ©.