2013-03-16 07:56:57

Serikali ya Tanzania yaombwa kukomesha vurugu za kidini na madhulumu kwa viongozi wa kidini


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro amemwelezea Rais Jakaya Mrisho Kikwete kama kiongozi anayelijali Kanisa Katoliki Tanzania na mwenye nia njema. Aidha, Kanisa hilo limesema kuwa Rais Kikwete amethibitisha katika muda wake wote wa uongozi wa Taifa la Tanzania kuwa ni kiongozi ambaye anawajali wanyonge na maskini.

Sifa hizo za kulijali Kanisa Katoliki na kuwa na nia nzuri na Kanisa hilo zilitolewa usiku wa Alhamisi, Machi 14, 2013 na Askofu Telesphor Mkude wakati wa hafla ya kuchangia ujenzi wa Parokia mpya ya Kigurunyembe iliyofanyika kwenye Bwalo la Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Magadu Officer’s Mess, nje kidogo ya mji wa Morogoro.

Akitoa neno la shukrani wakati akimkaribisha Rais Kikwete kwenye hafla hiyo na baada ya kukamilika kwa shughuli ya uchangiaji, Askofu Mkude alimwambia Rais Kikwete “Wewe Mheshimiwa Rais ni kiongozi ambaye unalijali Kanisa Katoliki. Una nia nzuri na Kanisa. Kigurunyembe ni sehemu ndogo sana ya nchi ya Tanzania ambayo wewe unaiongoza. Hata hivyo, umekuwa tayari kuacha yote yaliyo makubwa na kukubali kujishusha na kuja kuzungumza na hili kundi dogo la Kigurunyembe.”

Aliongeza Baba Askofu Mkude: “Kwa hili unatufundisha kwa vitendo maana ya kujali wanyonye na maskini. Baba Mheshimiwa umetujali sana. Mungu akubariki sana.” Alisisitiza Askofu Mkude: “Mwisho mgeni rasmi nirudie kwa kukushukuru na kusema kuwa yote haya yasingeliwezekana kama usingeliwepo wewe mwenye binafsi kwenye shughuli hii. Tunakushukuru kwa kutujali, kututhamini na kutupenda sisi kama raia wa nchi yako na ukaona ni bora ufike mwenyewe.”

Uchangiaji huo wa ujenzi wa parokia mpya ya Kigurunyembe ulilenga kukusanya kiasi cha Sh. Milioni 200 lakini wachangiaji waliishia wakichangia kiasi cha Sh. Milioni 255 zikiwamo fedha taslim Sh. Milioni 73.

Katika neno lake, Askofu Mkude pia aliwashangaa watu ambao wamekuwa wanachoma makanisa nchini kwa visingizio vya dini akisema kuwa taasisi na majengo yanajengwa kwa thamani kubwa na kama kweli Watanzania wanapenda maendeleo ni lazima waache kuchoma majengo yanayojengwa kwa thamani kubwa.

“Mtapata wapi maendeleo kwa kuchoma taasisi na majumba ambayo tayari tumeyajenga tena kwa gharama kubwa sana?” aliuliza Askofu Mkude na kumtaka Rais Kikwete kuchukua hatua za kukomesha fujo na vurumai za kidini nchini pamoja na kuuawa kwa viongozi wa dini.

“Haya siyo mazoea yetu kama ulivyosema wewe Mheshimiwa Rais katika hotuba yako ya mwezi Januari mwaka huu. Huu siyo utamaduni wetu. Ni lazima tukubali kurudi kuishi katika haki, katika amani na katika heri. Tunakuomba utusaidie makanisa yetu yasichomwe moto. Utusaidie viongozi wetu wasiuawe Mheshimiwa Rais.”










All the contents on this site are copyrighted ©.