2013-03-16 11:53:25

Ratiba elekezi ya Papa Francis kuanzia tarehe 17 hadi 24 Machi 2013


Ifuatayo ni Ratiba Elekezi ya shughuli muhimu zinazotarajiwa kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francis kuanzia Jumapili tarehe 17 hadi tarehe 24 Machi 2013. Jumapili tarehe 17 Machi 2013, saa 4:00 asubuhi, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Anna, iliyoko ndani ya Mji wa Vatican. Baadaye, atasali Sala ya Malaika wa Bwana na waamini, mahujaji na watalii watakaokuwa wamefika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, majira ya saa 6:00 mchana kwa saa za Ulaya.

Jumatatu, tarehe 18 Machi 2013, saa 6:50 mchana anatarajiwa kukutana na Rais wa Argentina kwenye Makao yake ya muda yaliyoko Domus Sanctae Marthae.

Jumanne, tarehe 19 Machi 2013, saa 3:30 asubuhi ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, mwanzo wa utumishi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Atapata pia nafasi ya kuzungumza na wawakilishi wa Serikali watakaohudhuria tukio hili la kihistoria na baadaye, atapata chakula cha mchana na wageni waalikwa kule Domus Sanctae Marthae.

Jumatano tarehe 20 Machi 2013 kwenye Ukumbi wa Clementina, atazungumza na viongozi wawakilishi wa madhehebu na dini mbali mbali, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu katika kuwahudumia watu, kwa pamoja wakipania kujenga umoja na udugu, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Ijumaa, tarehe 22 Machi 2013 Baba Mtakatifu Francis atakutana na kuzungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa nchi na Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.

Jumamosi, tarehe 23 Machi 2013 ataondoka kwa Elkopta kuelekea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na huko watapata chakula cha pamoja na baadaye atarudi Vatican.

Jumapili, tarehe 24 Machi 2013, Jumapili ya Matawi na Siku ya Vijana Kijimbo, Baba Mtakatifu Francis kwa mara ya kwanza, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye kusali Sala ya Malaika wa Bwana.







All the contents on this site are copyrighted ©.