Papa Francis ni Baba wa Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya
Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anampongeza Baba Mtakatifu Francis
kwa kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kwa waamini wapatao Billioni 1.2, walioenea
sehemu mbali mbali duniani, baada ya siku mbili za kikao cha Conclave kilichokuwa
kinafanyika kwenye Kikanisa cha Sistina, mjini Vatican.
Caritas Internationalis
inaungana na Watu wa Familia ya Mungu kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu
Francis, ina Sali pia kwa ajili ya ulimwengu mzima, ili kujenga na kuimaarisha mshikamano
wa kidugu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.
Caritas inasema kwamba, Papa Francis
ni Myesuit wa kwanza kabisa kuwahi kuchaguliwa kuwa Papa tangu Shirika hili lilipoanzishwa
na Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Ni Kiongozi wa kwanza kabisa katika historia ya Kanisa
kuchaguliwa kutoka miongoni mwa waamini wa Amerika ya Kusini. Ni kiongozi ambaye amejipambanua
kwa kuchangia huduma kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Ameonesha
upendo wa pekee kwa wagonjwa na waathirika wa Ukimwi, kiasi cha kuwaosha miguu kwa
upendo wa kibaba.
Kardinali Oscar Maradiaga anasema, si bure kujitwalia jina
la Mtakatifu Francis, kwani Francis wa Assisi alijimbanua kwa mshikamano wake makini
na thabiti kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, kiasi
hata cha kuacha utajiri na fahari ya nyumbani kwake, ili kushiriki katika ujenzi wa
Kanisa la Kristo, kwa njia ya huduma makini na ya kina kwa maskini wa nyakati zake.
Caritas inaona kwamba, hapa kwa hakika “upele umepata mkunaji”. Papa Francis
anatarajiwa kuwa mdau mkuu katika kutafuta, kutetea na kudumisha haki jamii, kwa kutoa
kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili dunia
iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Ni changamoto ya kuendelea kudumisha
haki, amani, umoja na udugu, kama alivyosema Papa Francis alipoonekana hadharani kwa
mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Baba wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba,
Caritas ni mdau mkubwa wa huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa sehemu mbali
mbali za dunia, bila ubaguzi, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.