Dira: Usiwasahau Maskini, dumisha amani na utunzaji bora wa mazingira!
Baba Mtakatifu Francis, Jumamosi, tarehe 16 Machi 2013 amewashukuru na kuwapongeza
wanahabari kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wamekuwa wakifuatilia matukio
muhimu ya Kanisa tangu pale Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipoamua kwa
utashi na uhuru kamili kung'atuka kutoka madarakani. Amepongeza kazi kubwa inayofanywa
na vyombo vya mawasiliano ya Jamii katika ulimwengu wa utandawazi.
Baba Mtakatifu
Francis anawapongeza wanahabari waliofanya kazi zao usiku na mchana kuwahabarisha
watu kile kilichokuwa kinatendeka mjini Vatican, kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro.
Wamepata nafasi ya kuweza kusimulia kuhusu Vatican, Kanisa, Ibada na Mapokeo yake,
Imani; Dhamana na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hili ni tukio la imani linalopaswa
kutazamwa katika mwono wa imani, ili kuweza kutoa taarifa kamili kwa hadhira inayokusudiwa.
Ni tukio kwa ajili ya watu wa Mungu wanaofanya hija ya kumwendea Yesu Kristo. Kwa
kuwa na ufahamu huu, ndipo mtu anavyoweza kung'amua mantiki ya maisha na utume wa
Kanisa.
Baba Mtakatifu Francis anabainisha kwamba, Kristo ndiye mchungaji mkuu
wa Kanisa anayeendelea kuwapo katika historia kwa njia ya uhuru wa binadamu. Kati
ya watu wengi, kuna mmoja anayechaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini
ikumbukwe kwamba, mhusika mkuu ni Yesu Kristo ambaye ni rejea ya Kanisa na bila Kristo
hakuna Kanisa na wala akina Petro na ndugu zake wasingakuwepo! Kristo yupo na anaendelea
kuliongoza Kanisa lake hadi utimilifu wa dahali.
Baba Mtakatifu Francis anasema
kwamba, matukio yote yaliyotendeka ndani ya Kanisa kwa siku za hivi karibuni, mhusika
mkuu ni Roho Mtakatifu; ndiye aliyemwongoza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
kung'atuka kutoka madarakani, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa. Anamshukuru
kwa uwapo wake kwa njia ya Sala na tafakari ya kina, iliyowaongoza Makardinali wakati
wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kanisa lina asili mbili: ile ya
Kimungu na kibinadamu; ina karama na mapungufu yake, lakini linatambua dhamana na
wajibu wake katika maisha ya mwanadamu, changamoto kwa wanahabari kujitahidi kuwapatia
watu mwanga wa matukio haya, daima wakijitahidi kukumbatia ukweli, matashi mema na
uzuri unaolifanya Kanisa kuendelea kutangaza ukweli, utashi na uzuri wa binadamu.
Kila mtu anaalikwa kutangaza mambo haya msingi na wala si kujitangaza mwenyewe!
Jina
Francis ambalo analitumia anasema ni changamoto iliyotolewa kwake na Kardinali Claudio
Hummes, baada ya kuona kwamba, amechaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, akamwambia, usiwasahau maskini. Hapa wazo la Mtaka Francis wa Assisi likamjia
kichwani kwake, kwani ni mtu ambaye alipenda kudumisha amani na utunzaji bora wa mazingira.
Mtu ambaye ana moyo na mwelekeo wa namna hii kwa hakika lazima ajikite katika maisha
ya ufukara.
Anawataka wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu
wa ndani; daima wakijitahidi kuifahamu Injili ya Kristo na hali halisi ya maisha na
utume wa Kanisa. Baada ya hotuba yake iliyokuwa inashangiliwa mara kwa mara, Baba
Mtakatifu Francis aliwaweka wanahabari waliokuwa wamefurika kwenye Ukumbi wa Paulo
wa sita, wakiwa na familia, ndugu na jamaa zao, chini ya uongozi na usimamizi wa Bikira
Maria.