2013-03-16 09:12:49

Baba Mtakatifu Francis anafungua ukurasa mpya wa matumaini ndani ya Kanisa


Mheshimiwa Padre Adolfo Nicolàs, Mkuu wa Shirika la Wayesuit kwa niaba ya Wanashirika wenzake, anapenda kumpongeza Baba Mtakatifu Francis kwa kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, tukio ambalo linafungua ukurasa mpya wa Kanisa, ukiwa umesheheni matumaini thabiti.

Kwa kutambua dhamana na utume aliokabidhiwa na Mama Kanisa, Shirika la Wayesuit, linamshukuru na kumpongeza na kuahidi kumsindikiza ndugu yao katika Kristo kwa njia ya sala, anapoliongoza Kanisa.

Jina Francis ambalo Baba Mtakatifu amechagulia kwa utashi wake mwenyewe kama kielelezo na mfano wa kuigwa, linaonesha ari na moyo wa Kiinjili, kwa kuwa karibu zaidi na maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii; ni utambulisho wake kwa watu wa kawaida, watu wasiokuwa na jina katika Jamii, watu wanaoangaliwa kwa jicho la makengeza. Hii ni dhamana nyeti inayopania kuleta mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.

Tangu siku ile ya kwanza alipojitokeza hadharani mbele ya umati mkubwa uliokuwa umefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameonesha hali ya unyenyekevu, mang’amuzi na uzoefu wa shughuli za kichungaji na mtu mwenye tasaufi ya kina.

Padre Nicolàs anabainisha kwamba, huu ni utambulisho wa Shirika lao na kielelezo makini cha maisha ya kitawa, yanayopata chimbuko lake katika utume na wito wa kipadre. Utajiri wote huu sasa unaunganishwa kwa ajili ya utekelezaji wa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kifungo cha upendo katika huduma.

Shirika la Wayesuit wanapenda kuungana na Kanisa zima ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani na wanaahidi kwamba, watashirikiana naye katika utekelezaji wa utume wake, wakitambua kwamba wao kama Wayesuit wanayo nadhiri ya nne inayowafunga kuonesha Utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.








All the contents on this site are copyrighted ©.