2013-03-15 07:58:20

WCC: Mabadiliko ya Tabianchi ni chanzo kingine cha uvunjifu wa haki msingi za binadamu


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema kwamba, mabadiliko ya Tabianchi yamekuwa ni chanzo kingine cha uvunjifu wa haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Kauli hii pia imesikika hivi karibuni wakati wa kikao cha ishirini na mbili cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki Msingi za Binadamu, kilichofanyika mjini Geneva. RealAudioMP3
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakazia kwamba, kuna haja ya kuwa na mikakati inayopania kudumisha haki na utunzaji bora wa mazingira, dhamana inayopaswa kuwashirikisha Mashirika ya Misaada ya Makanisa, Ushirikiano wa masuala ya kiimani pamoja na Vyama vya Kiraia.
Rèmy Pagani Mstahiki Meya wa Jiji la Geneva ambaye alikuwa ni kati ya wawezeshaji katika mkutano uliokuwa umeandaliwa na Baraza la Makanisa Duniani, aliwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira, kama sehemu ya mchakato wa kushiriki katika kuendeleza ile kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu. Jukwaa hili liwashirikishe watu wengi zaidi, kwani madhara na athari za mabadiliko ya tabianchi zinawakumba wote bila ubaguzi.
Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kupunguza maneno yanayotolewa kwenye Majukwa ya Kisiasa na kuanza kutekeleza sera na mikakati inayopania kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Ni mchango wa Dr. Mariyam Shakeela, Waziri wa Mazingira, nishati na Kaimu Waziri wa Jenda, Familia na Haki msingi za binadamu nchini Russia.
Anasema, makubaliano ya Umoja wa Mataifa katika mkutano wake wa Mazingira uliofanyika Rio kunako mwaka 1992, kimsingi Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa na mwono wa pamoja, lakini uwajibikaji tofauti, jambo ambalo linahitaji kuunda Jukwaa la Umoja wa Mataifa litakalokuwa na dhamana ya kutetea haki msingi za binadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ni kubwa sana kwa mamillioni ya watu ambao wanaendelea kutumbukia katika umaskini wa hali na kipato, baa la njaa na utapiamlo pamoja na magonjwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mabadiliko ya tabianchi yamepelekea ukame wa kukithiri, mafuriko na magonjwa ya milipuko. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwekeza katika kukusanya, kusoma na kusambaza takwimu zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Utekelezaji wa sheria zinazolinda haki msingi za binadamu zinapaswa kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira na misitu pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwa na soko mbadala litakalotoa bidhaa zinazoenzi uchumi wa kijani. Jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, inaibua mbinu mkakati wa kulinda Jamii zisizokuwa na uwezo wa kujihami kutokana na madhara ya Tabianchi.









All the contents on this site are copyrighted ©.