2013-03-15 14:32:50

Makardinali waahidi kushikamana na Baba Mtakatifu katika kulihudumia Kanisa


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya Makardinali wenzake, wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi aliyolijalia Kanisa lake kwa kulipatia mchungaji mkuu mpya. Wanamshukuru Baba Mtakatifu Francis kwa kukubali kujitwika dhamana ya kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Jambo linalohitajika zaidi ni upendo kwa Kristo katika kutekeleza dhamana ya kuliongoza Kanisa; dhamana nyeti na inayodai uwajibikaji wa hali ya juu. Lakini Makardinali wanatambua kwamba, Kristo Mchungaji mwema daima atakuwa kandoni mwake na ataendelea kumwangazia kwa njia ya Roho Mtakatifu ili aweze kulipyaisha Kanisa.

Makardinali wamemhakikishia mchango na mshikamano wa dhati wakati anapotekeleza utume wake katika Kanisa hili linaloendelea kupata mang'amuzi ya Pentekoste mpya, kila mtu akitenda na kutekeleza dhamana hii mintarafu neema, karama na baraka alizokirimiwa, ili Mwenyezi Mungu apewe sifa na utukufu.







All the contents on this site are copyrighted ©.