2013-03-15 08:17:47

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; upendo na mshikamano wa kidugu


Askofu msaidizi Euzebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anabainisha kwamba, Kwaresima ni kipindi kilichokubalika cha kufanya toba na wongofu wa ndani ili kumrudia Mwenyezi Mungu, tayari kutekeleza mapenzi yake. Ni kipindi cha kupiga moyo konde ili kuikimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, tayari kujipatanisha na Mungu, Kanisa pamoja na jirani.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea sehemu ya kwanza ya mahojiano na Askofu Eusebius Nzigilwa katika kipindi cha Kwaresima. RealAudioMP3

Mama Kanisa anawaalika waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima, kutoka katika dhambi na nafasi zake, kwa kugeuza mienendo ya maisha, kama inavyooneshwa katika Maandiko Matakatifu. Vielelezo vya toba anasema Askofu Nzigilwa ni: kufunga na kusali; kujiondoa katika anasa, kama alama ya unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kujenga na kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu.

Kufunga ni tendo la toba na wema kwa ajili ya jirani, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wajifunze kujinyima kwa ajili ya wahitaji zaidi kama kielelezo cha mshikamano wa kidugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.