2013-03-15 08:05:43

Kipindi cha Kwaresima kiwasaidie waamini kuwajibika katika utunzaji bora wa mazingira


Jumuiya ya Waanglikani Duniani katika Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 inawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda, kuheshimu na kutunza mazingira kwa kupunguza hewa ya ukaa wanayozalisha majumbani, viwandani na maeneo yao ya kazi, kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza kazi ya uumbaji. Itakumbukwa kwamba, Kwaresima ni muda muafaka uliokubalika wa kufanya: toba na wongofu wa ndani; kufunga na kusali; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kutekeleza matendo ya huruma. RealAudioMP3
Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kuondokana na mambo yote yanayokwenda kinyume na mapenzi na mpango wa Mungu kwa mwanadamu na viumbe wengine wote, kwani hata wao pia ni sehemu ya kazi ya Uumbaji. Waamini wa Kanisa Anglikani kwa namna ya pekee kwa Mwaka huu, wanaalikwa kujikita zaidi katika matendo ya huruma kutokana na sadaka ambayo wataifanya wakati wa Kipindi chote cha Kwaresima, Siku Arobaini za kutafakari: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Ile ni fursa kwa waamini kuangalia mchango wanaoweza kuchangia katika kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Siku arobaini zisaidie kuamsha changamoto na ari ya kulinda na kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa kuenzi kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu, lakini kutokana na ubinafsi na matumizi mabaya mazingira, dunia inaendelea kushuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabianchini. Kufunga na kujinyima ni sehemu ya mapokeo ya kipindi cha Kwaresima. Waamini wajifunze kujenga na kudumisha utamaduni wa kujinyima na kutoa sadaka kwa maskini na wahitaji zaidi. Kwa mwaka huu, waamini na watu wenye mapenzi mema, wajifunze kutoa sadaka kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa; kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha matumizi bora ya rasilimali ambayo waamini wamekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Mazingira bora ni kati ya zawadi kubwa ambazo mwanadamu amekabidhiwa, lakini hatima yake iko mashakani. Ikumbukwe kuwa kila mtu anachangamotishwa kujenga utamaduni wa kutunza mazingira; watu wajifunze kubana matumizi ya maji wanayotumia, kwani maji ni uhai. Inawezekana kabisa kupunguza matumizi ya umeme na gasi majumbani na ofisini. Unaweza kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kutumia usafiri wa umma badala ya kuendesha gari binafsi.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha kumrudia Mwenyezi Mungu kwa moyo mkuu. Yale ya kale yaliyoharibu uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, yazikwe kwenye majivu wanayopakwa waamini Jumatano ya Majivu. Waamini wakimbilie wema na huruma ya Mungu kwa njia ya kufunga, toba na matendo ya huruma kwani Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, atawapokea na kuwasamehe dhambi zao. Kila mtu akithubutu, inawezekana kulinda na kutunza mazingira, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.








All the contents on this site are copyrighted ©.