Changamoto kuu: ni kutembea, kujenga na kumuungama Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka!
Baba Mtakatifu Francis, Alhamisi tarehe 15 Machi 2013, Jioni, ameadhimisha Ibada ya
Misa Takatifu kwa ajili ya kuliombea Kanisa akishirikiana na Makardinali walioshiriki
katika uchaguzi wa Papa Mpya kwenye Kikanisa cha Sistina, mjini Vatican. Katika mahubiri
yake kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia mambo makuu matatu:
kutembea, kujenga na kuungama.
Familia ya Mungu inaalikwa kutembea katika mwanga
wa Mungu, kwa kutambua kwamba, maisha ya kila mwanadamu ni hija inayomwajibisha kutekeleza
mapenzi ya Mungu katika maisha yake kama alivyofanya kwa Mzee Ibraham, Baba wa Imani
na hatimaye, Mwenyezi Mungu akamtekelezea ahadi zake.
Baba Mtakatifu Francis
anasema, waamini lazima wajitambue kwamba wao ni mawe hai na hivyo wanachangamotishwa
kulijenga na kuliimarisha Kanisa, wakiwa wameungana na Roho Mtakatifu. Ni mwaliko
wa kulijenga Kanisa ambalo ni mchumba amini wa Kristo, juu ya Jiwe kuu la pembeni
ambalo ni Kristo mwenyewe.
Familia ya Mungu katika hija ya maisha yake hapa
duniani inaalikwa kufanya hija pamoja na Kristo ili kumshuhudia Kristo kwa njia ya
sala na matendo thabiti, vinginevyo waamini wanaweza kujikuta wakimtumikia shetani
na hatimaye kumezwa na malimwengu.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francis
anawaalika waamini kutembea, kujenga, kuimarisha na kushuhudia; dhamana ambayo si
rahisi kuitekeleza kutokana na ukweli kwamba, kuna wakati ambapo waamini wanaweza
kukumbana na vikwazo pamoja na vizingiti vinavyoweza kuwafanya kushindwa kusonga mbele
zaidi. Waamini wajitahidi kuungana na Mtakatifu Petro ambaye alimuungama Yesu kuwa
ni Mwana wa Mungu aliye hai, ingawa mwanzoni alitishika kwa uwepo wa Msalaba!
Baba
Mtakatifu Francis anasema kwamba, Waamini hawawezi kufanya hija na kupania kulijenga
Kanisa bila ya kuukumbatia Msalaba, kwani mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha ufuasi
wa Kristo, haijalishi wewe una nafasi gani katika Kanisa. Hija ya mfuasi wa Kristo
inaambatana na Msalaba. Papa anawaalika Makardinali baada kusali na kutafakari wakati
wote walipokuwa kwenye uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, sasa wanapaswa kuwa
na ujasiri wa kutembelea mbele ya Kristo kifua mbele huku wakiwa wameukumbatia Msalaba.
Hii
ni changamoto ya kulijenga Kanisa juu ya Damu Azizi ya Yesu iliyomwagika pale juu
Msalabani; kuungama ukuu wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka, kwa njia hii Kanisa
litazidi kusonga mbele. Baba Mtakatifu Francis amewatakia Makardinali wote nguvu ya
Roho Mtakatifu kwa maombezi ya Bikira Maria, ili kwa pamoja waweze kutembea, kujenga
na kumshuhudia Yesu Kristo Mteswa!
Katika sala za Waamini, Kanisa limesali
kwa ajili ya kumwombea Khalifa wa Mtakatifu Petro Mpya pamoja na Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita, ili aendelee kulihudumia Kanisa katika maisha ya sala na
tafakari. Wamewaombea viongozi wa kimataifa kutumia vyema madaraka yao kwa ajili ya
mafao ya wengi na wala si kwa ajili kujitafuta wenyewe au kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Kanisa limewaombea pia wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze
kufarijiwa na hatimaye, kupewa taji la utukufu.
Mara baada ya Maadhimisho ya
Fumbo la Ekaristi Takatifu, Papa Francis alikwenda kutembelea makazi yake mapya ambayo
kwa sasa yanaendelea kufanyiwa ukarabati mdogo.