2013-03-15 10:07:48

Baba Mtakatifu Francis ni ushuhuda makini wa Ukatoliki usiokuwa na mipaka!


Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemtumia Baba Mtakatifu Francis ujumbe wa matashi mema, kwa niaba yake mwenyewe na kwa niaba ya wananchi wa Italia katika ujumla wao. Anasema kwamba, anatambua na kuheshimu utajiri mkubwa wa maadili na kitamaduni unaofumbatwa katika Kanisa; tunu msingi ambazo zinasimamiwa pia na Serikali ya Italia.

Mtakatifu Francis ni msimamizi wa Italia; jina ambalo linaonesha pia utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho, ndilo jina ambalo Papa ameamua kulichagua kama utambulisho wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Rais Napolitano anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francis kwa maneno aliyoyasema wakati alipoonekana kwa mara ya kwanza hadharani mara baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.

Serikali ya Italia inapania kuendeleza ushirikiano wa dhati na Vatican, kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, haki msingi za binadamu, haki jamii, amani, utu na heshima ya kila mtu. Rais Napolitano ametumia fursa hii pia kumshukuru Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyeliongoza Kanisa kwa uchaji na hekima ya hali ya juu; na kwamba, walijenga jukwaa la majadiliano na uhusiano wa karibu katika maisha ya kiroho.

Rais Giorgio Napolitano anasema, Baba Mtakatifu Francis analeta mjini Roma ushuhuda wa Ukatoliki usiokuwa na mipaka; utume wa maisha ya kiroho na kichungaji kwa waamini na kwamba, haya ni mang'amuzi yanayoletwa kwa mara ya kwanza kutoka Amerika ya Kusini. Mwishoni, Rais Napolitano anamtakia kila la kheri na baraka tele katika utekelezaji wa majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.