2013-03-14 15:41:40

Ijue afya ya figo zako!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewahimiza Watanzania kuwa na tabia ya kunywa maji mengi kila siku ili kujikinga na matatizo ya figo ambayo yanazidi kuongezeka kila siku.
Ametoa wito huo Alhamisi, Machi 14, 2013, wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Arusha waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya ya Figo Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya AICC jijini humo.
Kaulimbiu ya Siku ya Afya ya Figo Duniani mwaka huu ni “Figo Salama kwa Maisha yako: Epusha Madhara Makubwa kwa Figo” au “Kidneys for Life: Stop Acute Kidney Injury”
Waziri Mkuu alisema mtoto wa miaka 10 hadi mtu mzima wanatakiwa wanywe maji kiasi kisichopungua lita moja na nusu kwa siku wakati mtoto mwenye mwaka mmoja anatakiwa anywe maji yasiyopungua nusu kikombe (sawa na mililita 100) na kwamba kiasi hicho huongezeka kadri umri wa mtoto unavyoengezeka. “Hii itasaidia kuhakikisha hawaishiwi maji mwilini,” aliongeza.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, imekadiriwa kuwa watu milioni mbili hupoteza maisha kila mwaka kutokana na maradhi ya ghafla ya figo wakati asilimia 20 ya vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini husababishwa na maradhi hayo.
“Wataalam wanasema maambukizi ya magonjwa hayo husababisha madhara makubwa ya figo (Acute Kidney Injuries) ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa utendaji kazi wa figo. Hali hiyo husababisha watu kupata ugonjwa wa ghafla wa figo (mshtuko wa figo) na pia kusababisha athari kubwa kwenye figo na kuzifanya zishindwe kufanya kazi ipasavyo,” alisema.
Alisema maradhi yanayoweza kujitokeza ghafla na kuharibu figo hayajatiliwa mkazo ipasavyo, hasa katika nyanja za utoaji mafunzo ya tiba, utafiti na elimu ya afya ya figo kwa umma. “Hali hii husababisha kutotumika kikamilifu kwa fursa za kubaini maradhi yanayojitokeza ghafla na kuharibu figo; pia inaathiri utoaji huduma za afya ya figo usiokidhi, na hivyo wagonjwa kulazwa kwa muda mrefu hospitalini,” alisititiza.
Akifafanua umuhimu wa kuwepo haja ya upimaji afya ya figo, Waziri Mkuu alisema Machi, 2011 Taasisi ya Figo Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitoa huduma ya bure na kuwachunguza watu 3,500 ambapo watu 1,200 walikutwa na magonjwa ya figo.
“Mwaka huu 2013 katika maadhimisho yanayoendelea katika Jiji la Arusha, yaliyoanza Machi 11, 2013, jumla ya watu 2,020 kufikia saa 7.00 mchana jana walisajiliwa na kati yao 1,640 walifanyiwa uchunguzi. Kati yao wananchi 37 walipatikana na maradhi ya figo, wengine 219 walipatikana na matatizo ya shinikizo la juu la damu. Wananchi 65 kati ya 141 waliofanyiwa uchunguzi kwa kipimo cha Ultra Sound na walikutwa na matatizo. Jumla ya wananchi 63 walifanyiwa uchunguzi wa moyo wakwa vipimo vya ECHO na ECG.
Alisema jukumu kubwa kwa upande wa Serikali ni kuhakikisha kuwa fedha, vifaa, vifaa tiba na dawa za kukabiliana na ugonjwa wa mshtuko wa figo vinapatikana kwa wakati ili kulinda afya ya jamii. “Katika kudhihirisha azma hii ya Serikali, tayari tuna Kitengo cha Huduma za Tiba ya Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kitengo hiki kinatoa huduma kwa wagonjwa wote wanaohitaji huduma za tiba ya magonjwa ya figo. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanzisha utoaji wa huduma za tiba ya magonjwa ya figo. Ninazo taarifa kwamba, pale Dodoma kuna mashine za kisasa 10 za kusafishia damu.”
Alisema hospitali za rufaa za Bugando, KCMC na Mbeya ziko kwenye hatua mbalimbali za maandalizi ya kuanzisha huduma za tiba ya magonjwa ya figo. “Matarajio ni kwamba, kuwepo kwa huduma hizo kutaliwezesha Taifa katika kupambana na magonjwa ya figo,” aliongeza.
Alikemea tabia ya baadhi ya watu kujiamulia kununua dawa na kumeza bila kufanyiwa uchunguzi wa kitatibu na kuonya kuwa kuwa tabia hiyo inaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.
“Tuwaelimishe Watanzania umuhimu wa kuhakikisha kuwa wagonjwa wanaougua maradhi mengine wanapelekwa hospitali na wanapata tiba sahihi kwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya. Vilevile, ni vizuri kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara tuonapo dalili za ugonjwa ili kupatiwa tiba inayostahiki mapema,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alizindua Programu ya Ujumbe Mfupi wa Simu ya Mkononi (SMS) ya IJUE AFYA YA FIGO YAKO kwa kutuma ujumbe wenye neno FIGO kwenda namba 15021 kupitia mtandao wa simu wa Tigo ambapo mhusika atajibu maswali kadhaa na kupatiwa taarifa.
Aliishukuru kampuni ya simu ya mkononi ya Tigo kwa kutoa huduma hiyo bure na kuwasihi wananchi waitumie ili kupata taarifa juu ya afya ya figo zao.
Naye Mwenyekiti waTa asisi ya Figo Tanzania, Jaji Frederick Werema, aliwasihi Watanzania kujitolea kwa hali na mali kuiunga mkono taasisi hiyo ili iweze kufanya shughuli zake kwenye mikoa mingi zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.