Baba Mtakatifu Francis ni kiongozi anayetaka kutoa huduma kwa Kanisa la Kristo!
Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Kanisa limempokea
kwa mikono miwili, Baba Mtakatifu Francis anayetoka Amerika ya Kusini ambako kwa sasa
Kanisa lina waamini wengi wenye fursa na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa.
Uchaguzi wa Jina la Francis una maana kubwa katika maisha na utume wa Papa
Francis, jina amblo kwa mara ya kwanza linatumika katika historia ya Kanisa kwa ajili
ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni jina linalobainisha unyofu na ushuhuda wa Kiinjili,
mambo ambayo yamejionesha kwa Baba Mtakatifu alipotokeza hadharani kwa mara ya kwanza
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo Jumatano tarehe
13 Machi 2013.
Ameonesha unyenyekevu wa hali ya juu kwa kuomba sala na baraka
kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kabla hata ya Yeye mwenyewe kuwapatia
baraka yake ya kitume! Ni mtu wa sala, kama ilivyojionesha pia wakati akizungumza
na waamini wa Jimbo kuu la Roma. Inapendeza kuona Familia ya Mungu inasali kwa pamoja.
Baba
Mtakatifu Francis ni Myesuit na Wayesuit wanajipambanua na Watawa wa Mashirika mengine
kwa njia ya huduma kwa Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji
waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Uongozi
ni huduma na wala si uchu wa madaraka!
Huu ndio mwelekeo unaoneshwa na Kanisa
kwa wakati huu kwamba, watu wanaalikwa kuhudumia na kwamba Baba Mtakatifu Francis
ni mtu anayeonesha kwamba, kweli anataka kulihudumia Kanisa, kwani uchaguzi wake umekuja
wakati ambapo Papa Benedikto wa kumi na sita, alipoamua kung'atuka madarakani, kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha huduma kwa Mungu na jirani, kwa kutambua uwezo na umri
wake.
Baba Mtakatifu Francis amezungumza tayari kwa njia ya simu na Papa mstaafu
Benedikto wa kumi na sita na kwamba, anaendelea kumwombea katika utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro.