Wasindikizeni Makardinali kwa njia ya sala ili Kanisa liweze kupata Nahodha Mpya atakayeliongoza
Kanisa!
Askofu Richard Smith, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada anawaalika waamini
nchini humo kuungana na waamini wengine duniani kwa ajili ya kusali ili kuombea mafanikio
katika mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; ili Kanisa liweze kumpata
kiongozi atakeyafaa kuendeleza Jahazi la Mtakatifu Petro, baada ya Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, kuamua kwa utashi na uhuru kamili kung'atuka kutoka madarakani.
Askofu
Smith anawaambia waamini nchini Canada kwamba, katika kipindi hiki cha uchaguzi wa
Papa Mpya, watasikia mengi, lakini jambo la msingi kwa wao ni kulichukulia tukio hili
kwa jicho la imani, kwa kusali na kutafakari dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro
katika maisha na utume wa Kanisa.
Ni wajibu wao kuwaombea Makardinali ili
waweze kuwa na ujasiri wa kumchagua yule ambaye atakabidhiwa funguo za ukulu wa Mtakatifu
Petro; kwa kutambua kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha umoja na mshikamano
wa Kanisa. Ni kiongozi ambaye atakuwa na dhamana ya kuwafundisha: Imani, Maadili na
Sala.
Kardinali atakayedhaminishwa dhamana ya kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu
Petro wa 265, atapaswa kuwa ni kielelezo cha ushuhuda makini wa imani na changamoto
ya kutubu na kuongoka. Matukio yote haya yanayoendelea ndani ya Kanisa katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, yawaimarishe waamini katika: Sala, Tafakari na Matendo ya huruma;
wajitahidi kushikamana zaidi katika kipindi hiki cha neema.