2013-03-13 09:40:10

Mikakati ya kuimarisha tunu bora za maisha na wito wa familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia, hivi karibuni alizundua matarajio ya Baraza la Kipapa la Familia baada ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yaliyofanyika Jimbo kuu la Milano, Mei 2012.

Tukio hili ambalo lilikusanya Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lilidhihirisha umuhimu wa Familia katika Jamii na Kanisa, licha ya matatizo na magumu ambayo familia nyingi zinaendelea kukumbana nayo katika maisha na utume wake kwenye ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Lakini bado familia inabaki kuwa ni rasilimali kuu katika Jamii, kama tafiti nyingi zinavyobainisha kwamba, hapa ni mahali ambapo watu wengi wanapenda kukimbilia kwa ajili ya kupata faraja, amani na utulivu na kwamba, familia ni tarajio la vijana wengi ambao pia wameonesha kwamba, wanapenda kuishi katika ndoa kadiri ya Mafundisho ya Kanisa.

Huu ni ukweli unaoibuliwa kutoka katika undani wa mwanadamu, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na shinikizo linalooneshwa na baadhi ya watu kutaka kushabikia vitendo vinavyokwenda kinyume cha utu na maadili mema; hawa ni wale wanaotaka kufunga ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo linaonekana kuwa ni fashion kwa nchi nyingi za Ulaya. Ubinafsi ni kati ya vikwazo vinavyoendelea kudumaza tunu msingi na maisha yakifamilia.

Jambo la pili anasema Askofu mkuu Paglia ni watu kutaka uhuru usiokuwa na mipaka; uhuru usiozingatia maadili na utu wema; ni uhuru ambao kimsingi hautaki kuwajibika. Lakini ikumbukwe kwamba, familia ni taasisi inayowajibisha na kufungamanisha watu katika kifungu cha upendo mkamilifu. Madhara ya utandawazi yanapelekea baadhi ya watu kujitafuta wenyewe kiasi kwamba, hawana tena habari za kutaka kuishi pamoja kama Bwana na Bibi kadiri ya mpango wa Mungu sanjari na kulea watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kanisa linaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu kweli za Kiinjili, kwa kutambua kwamba, Familia ni Habari Njema ya watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo na kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia: Kwa hakika, watu wengi wanashindwa kuonja upendo, kiasi kwamba, wanajikuta wakielemewa na upweke hasi.

Kanisa lina uzoefu na mang’amuzi makubwa katika hija ya maisha ya mwanadamu. Linatambua ni kwa kiasi gani watu wanaendelea kuathirika kutokana na kumezwa mno na malimwengu pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo; hali inayowafanya kutetea vitendo vya utoaji mimba, kifo laini bila kusahau mateso na mahangaiko wanayopata wazee wasiokuwa na msaada kutoka katika familia zao.

Kanisa linatambua kwamba, Familia inaundwa kati ya Bwana na Bibi na Watoto ni matunda ya uhusiano wa dhati kati ya mume na mwanamke na kwamba, watoto hawa wanahitaji kulindwa, kuheshimiwa na kuelimishwa. Ndiyo maana Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utambulisho wa familia kadiri ya mpango wa Mungu, dhidi ya tabi ana tamaduni zinazotaka kudhalilisha mwono huu kwa kutaka kukumbatia ndoa za watu wa jinsia moja. Hili ni jambo ambalo kwa sasa linaendelea kupigiwa debe katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Kanisa kwa njia ya mikakati yake ya kichungaji, litaendelea kuenzi tunu bora za maisha ya kifamilia pamoja na kuitetea taasisi hii katika majukwaa ya kimataifa; kwa kuangalia pia tamaduni, ili tamaduni hizi ziweze kuenzi tunu bora na maisha ya kifamilia, ili ziweze kuleta mvuto na mguso katika maisha ya watu wengi ndani ya Jamii. Familia inapaswa pia kuangaliwa katika mtazamo mpana zaidi, kwa kukumbatia familia yote ya binadamu inayoundwa na watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema kwamba, Baraza la Kipapa la Familia kwa sasa linajiandaa kwa ajiliya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yatakayofanyika Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, kunako Mwaka 2015. Katika kipindi hiki chote cha maandalizi, kutafanyika tafakari ya kina kuhusu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya iliyofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba 2012 pamoja na Mafundisho ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa viongozi waandamizi na hotuba yake kwa Mahakama kuu ya Vatican.

Mwaka 2013 Jumuiya ya Kimataifa inajiandaa kuadhimisha Miaka 30 tangu Baraza la Kipapa la Familia lilipochapisha kwa mara ya kwanza Tamko la Haki za Familia na Miaka 20 tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzisha Siku ya Familia Kimataifa. Tamko hili litawasilishwa kwenye Umoja wa Mataifa na kwenye Makao Makuu ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva bila kusahau Bunge la Ulaya.

Baraza la Kipapa la Familia linaandaa Kongamano la Kimataifa la Wanasheria Wakatoliki litakalofanyika mjini Vatican mwishoni mwa Mwezi Juni, 2013. Lengo ni kuwajengea uwezo wasomi na wanazuoni kutafakari kwa kina kuhusu haki za familia katika mapambazuko ya Karne ya 21. Mkutano mkuu wa Baraza utakaofanyika mwezi Oktoba 2013 utatafakari tena Tamko la Haki za Familia; ili ziweze kufahamika na kusambazwa zaidi. Kuna maandalizi maalum ya semina zitakazokuwa zinajadili umuhimu wa majadiliano ya kifamilia, kwa kuwashirikisha mabingwa kutoka medani mbali mbali za maisha ya kijamii, ili kwa pamoja kuangalia kwa makini changamoto zinazoibuliwa katika maisha ya ndoa na familia.

Familia ni taasisi ya kwanza; changamoto katika elimu na makuzi; wazee na tasaufi ya wazee pamoja na dhana ya ushirikishwaji, ni baadhi tu ya mada zinazoendelea kupikwa na Baraza la Kipapa la Familia, kama anavyobainisha Askofu mkuu Vincenzo Paglia wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, zinatarajiwa kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuanzia tarehe 26 hadi 27 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, ili kwa pamoja kuweza kumshukuru Mungu kwa zawadi, maisha na utume wa Familia kama chombo cha kufundisha na kurithisha imani katika Jamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.