Macho ya waamini yameelekezwa kwenye Kikanisa cha Sistina
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne tarehe 12 Machi 2013
ulifurika umati wa waamini, mahujaji na watalii kushuhudia Makardinali wakila kiapo
na hatimaye kuanza mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Licha ya hali
mbaya ya hewa, lakini waamini wakiwa na miamvuli yao, waliendelea kusubiri kwa hamu
kufahamu walau matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa Papa Mpya.
Ilikuwa ni saa
1: 41 Usiku, kwa saa za Ulaya, sauti kubwa ilipotanda Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro kwa kuona moshi mweusi, dalili kwamba, bado Makardinali walikuwa hawajafulu
kumchagua Papa Mpya.
Makardinali 115 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura,
Jumatano wameendelea na ratiba yao kama kawaida kwa kupiga kura mara nne, yaani kura
mbili asubuhi na kura nyingine mbili nyakati za jioni. Maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya mawasiliano yamewawezesha mamillioni ya waamini na watu wenye mapenzi mema kufuatilia
mchakato wa uchaguzi wa Baba Mtakatifu moja kwa moja kutoka katika Kikanisa cha Sistina,
tangu pale Makardinali walipoanza maandamano kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu
Paulo, walipoingia kwenye Kikanisa cha Sistina, wakaanza kula kiapo hadi pale Monsinyo
Guido Marini alipofunga lango la Kikanisa cha Sistina, ili kutoa nafasi kwa Makardinali
kuanza rasmi mchakato wa kupiga kura.
Kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro, kuliwekwa Televisheni kubwa nne, zilizowawezesha waamini kufuatilia hatua kwa
hatua mchakato mzima wa Conclave, hadi pale moshi mweusi ulipotoka. Ilikuwa ni nafasi
kwa waamini pia kuwatambua Makardinali kwa sura kwani wengi wao wamesikika kwa majina,
lakini ni wachache waliokuwa wanafahamika zaidi. Katika matukio kama haya havikosekani
vituko! Lakini, macho na imani ya watu wengi ni kufahamu nani kati ya Makardinali
amechaguliwa kuliongoza Kanisa.