2013-03-12 08:06:58

Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa


Sakramenti ya upatanisho ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni jukwaa makini la Uinjilishaji Mpya; mahali ambapo waamini wanapata fursa ya kuweza kuunda dhamiri nyofu kwa kutambua jema la kufuata na baya la kuachana nalo! RealAudioMP3
Ni wajibu wa waamini kutambua umuhimu wa kupokea rehema kamili na rehema za muda; kwa kuyafahamu na kutimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanabahatika kufanya hija ya maisha ya kiroho wakiwa thabiti katika imani.
Haya ni baadhi ya mambo yaliyojadiliwa wakati wa Semina ya Ishirini na Nne iliyokuwa imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Toba, iliyohitimishwa hapo tarehe 8 Machi 2013, hapa mjini Vatican. Semina hii imehudhuriwa na Makleri 550 kama sehemu ya majiundo endelevu katika utume wao unaowapatia dhamana ya kuwaondolewa waamini dhambi zao, ili kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Washiriki wa Semina hii wamepata fursa pia ya kujadili mada za kimaadili, kanuni na sheria za Kanisa hasa kuhusiana na Sakramenti ya Upatanisho.
Ni semina ambayo inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, unaoendelea kutekeleza changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya pamoja na umuhimu wa ushuhuda wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha imani tendaji. Waamini wajenge utamaduni wa kupokea mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu, unaohitaji toba na wongofu wa ndani, ili kufurahia maisha ya imani, pamoja na kujifunga kibwebwe kutangaza kweli za Kiinjili, zinazogusa mioyo ya waamini ambao wanazipokea kwa upendo wa kimungu.
Mapadre watambue kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto ya kutoa nafasi ya kutosha katika mikakati na mipango yao ya kitume Parokiani na kwenye Vyama vya Kitume wanavyohudumia. Mapaadre pia wakumbuke kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio.
Kardinali Mauro Piacenza anasema kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni mahali ambapo waamini wakipatumia vyema panaweza kuwa ni msaada mkubwa katika Uinjilishaji Mpya; mahali ambapo imani inarithishwa na Mafundisho Tanzu ya Kanisa kubainishwa barabara.
Anasema, maungamo ni fursa makini ya kitaalimungu, ambayo mwamini anaweza kupata mang’amuzi ya ndani, kwa kuifia dhambi na hivyo kuonja maisha mapya kutoka kwa Kristo Mfufuka.
Kardinali Mauro Piacenza anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya Sakramenti ya Upatanisho; dhamana ya Uinjilishaji, Urithishaji wa imani pamoja na Mafundisho Tanzu ya Kanisa.
Hata pale kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi, bado Mama Kanisa anaendelea kuhimiza waamini kufanya toba, ndiyo maana dhamana ya Mtoa Toba mkuu inaendelea hata pale Ukulu wa kiti cha Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi! Hayo yamebanishwa na Monsinyo Krzysztof Nykiel, kiongozi mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Toba.
Semina hii imefanyika kwa wakati huu ambapo Mama Kanisa anaendelea kufanya hija ya kipindi cha Kwaresima kwa kukazia toba, wongofu wa ndani, umuhimu wa Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti pamoja na matendo ya huruma. Lengo ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Haya ni mambo yanayopaswa kujidhihirisha katika mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mapadre Maparokiani.








All the contents on this site are copyrighted ©.