Macho ya waamini na watu wenye mapenzi mema yanaelekezwa kwa sasa mjini Vatican
Katika mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hadi sasa kuna jumla ya
Makardinali 152 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi hiki cha Conclave
Makardinali watakaomsaidia Camerlengo ni: Kardinali Antonios Naguib, kutoka katika
kundi la Makardinali Maaskofu, Kardinali Marc Ouellet kutoka kundi la Mapadre na Kardinali
Francesco Monterisi kutoka katika kundi la Mashemasi.
Padre Federico Lombardi
anasema mkutano wa mwisho kabla ya Makardinali kuingia kwenye mchakato wa kumchagua
Papa Mpya umezungumzia umuhimu wa ukweli na uwazi katika masuala ya fedha na kwa namna
ya pekee, Benki ya Vatican.
Hii ni mada iliyopembuliwa na Kardinali Tarcisio
Bertone, ambaye kwa wadhifa wake ni Rais wa Dekania ya Makardinali wanao ratibu shughuli
za taasisi hii. Kwa sasa kuna mpango wa kimataifa unaoratibu shughuli za Benki ya
Vatican, ili kukazia ukweli na uwazi katika masuala ya fedha.
Makardinali
wameendelea pia kupembua wasifu wa Papa Mpya na Matarajio ya Kanisa baada ya uchaguzi
huu ambao unafuatiliwa na waamini wengi kwa njia ya sala, lakini pia kwa njia ya vyombo
vya upashanaji habari. Makardinali wakishamaliza dhamana ya kupiga kura na hatimaye
kumchagua Khalifa Mpya wa Mtakatifu Petro, moshi mweupe utatoka kwenye Kikanisa cha
Sistina na hapo kengele za Kanisa kuu la Mtakatifu Petro zitapigwa kuwaalika waamini
kuja kusikiliza na kumwona Papa Mpya. Tangu kengele zitakapopigwa hadi Papa Mpya kuonekana
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ni walau muda wa saa moja.
Itakumbukwa
kwamba, kuna jumla ya Makardinali 115 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati
wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Bado waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee,
kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi katika uchaguzi wa Papa Mpya unaoanza
rasmi tarehe 12 Machi 2013.