Jiografia ya Makardinali wanaoingia kwenye Conclave mjini Vatican
Wakati huu wa uchaguzi wa Papa Mpya jambo la msingi kukumbuka ni kwamba, Kanisa ni
moja, Takatifu, Katoliki, na la Mitume. Makardinali katika mwelekeo wa mawazo yao
ya jumla wamebainisha kwamba, wanataka kumchagua Kiongozi mkuu wa Kanisa atakayeliongoza
Kanisa la Kristo kama Baba mwenye huruma na mapendo, kielelezo cha umoja na mshikamano
wa Kanisa; kiongozi mwenye dhamana ya kulinda na kusimamia kweli za Kiinjili, Maadili
na utu wema. Haijalishi mahali anapotoka mtu, jambo la msingi ni kiongozi.
Kwa
jumla, kuna Makardinali 115 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wanaoanza mchakato
huu kwenye Kikanisa cha Sistina kwa kula kiapo, tafakari ya Neno la Mungu na uchaguzi
wa kwanza. Makardinali 60 wanatoka katika nchi za Ulaya, kuna Makardinali 33 kutoka
Amerika, Makardinali 11 kutoka Barani Afrika, Asia kuna Makardinali 10 na Oceania
kuna Kardinali mmoja. Itakumbukwa kwamba, kwenye Conclave ya Mwaka 2005, Kenya haikuwa
na Kardinali, lakini mwaka huu, Kardinali John Njue yupo.
Kuna Makardinali
40 ambao wametekeleza utume wao au bado wanaendelea kufanya shughuli mbali mbali mjini
Vatican. Kati ya Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura 67 ni wale walioteuliwa
na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Wastani wa umri wa Makardinali
wanaopiga kura ni kati ya miaka 71. Kardinali Walter Kasper mwenye umri wa miaka 80
ni kati ya wale waliobahatika kuingia katika Conclave wakiwa na umri mkubwa zaidi.
Kati ya Makardinali vijana wana umri wa miaka 54 na 56. Kardinali Luis Antonio Tagle
ana umri wa miaka 56.
Mwishoni, itakumbukwa kwamba, kundi la Makardinali Maaskofu
lina Makardinali 6; Kundi la Makardinali Mapatriaki lina jumla ya Makardinali 4; Kundi
la Makardinali Mapadre lina jumla ya Makardinali 153 na Makardinali Mashemasi wako
44. Kuna jumla ya Makardinali 207.