2013-03-11 07:56:37

Wanawake wanachangamotishwa kuwa waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa pamoja na familia zao!


Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewataka akinamama wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali kuwa waaminifu kwa wenza wao na wanafamilia wao ili waweze kupata ushirikiano kutoka kwao.

Alisema mbali ya majukumu mengi yanayowakabili, akinamama wanapaswa kuwa karibu na familia zao kwani ndiyo msingi mkuu wa Taifa. “Hatuna budi kutoa malezi mema kwa wenza wetu na watoto wetu. Tunapofanikiwa katika shughuli zetu, tusiache kuwa waaminifu kwa wana-familia wetu (akinababa na watoto wetu); tuwaheshimu na kuwaenzi kwa kuwashirikisha kazi tunazofanya ili tuweze kupata ushirikiano wao na baraka zao,” alisema.

Mama Pinda ametoa kauli hiyo Jumamosi, Machi 10, 2013 wakati akizungumza na wanawake wajasiriamali walioshiriki Maonyesho Maalum ya Batik (Batik Gala Night) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwenye ukumbi wa Hellenic Club, Upanga jijini Dar es Salaam.

Maonyesho hayo yaliandaliwa na Kamati ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali Tanzania (MOWE) kwa kushirikiana na Ofisi ya Shirika la Kazi Duniani hapa nchini (ILO) yalikuwa na nia ya kuamsha chachu ya kuendeleza kazi za akinamama wanaofanya maonyesho kila mwaka yaliyopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Alisema akinamama wanapaswa kuungana kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kuunganisha ujuzi, stadi walizonazo na kushirikishana uzoefu. Alisema hawana budi kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora wa kiwango cha juu ili waweze kukabiliana na ushindani kwenye soko.

“Napenda kusisitiza, suala la ubora wa bidhaa tunazozizalisha kwa kuzingatia viwango vya Kitaifa na kimataifa ili bidhaa zetu ziweze kupata uhakika wa soko. Hili litafanikiwa pia endapo tutazingatia pia ubora wa vifungashio tunavyotumia kwenye bidhaa zetu. Endapo, tutazingatia viwango, vifungashio na kutumia kiandishi-anuani (barcodes), sioni ni kwa nini bidhaa zetu zisiende hadi masoko ya mbali huko ughaibuni,” alisema.

Aliwataka akinamama wajipange vizuri kwa ajili ya Maonyesho makubwa ya kitaifa (MOWE) yatakayofanyika Oktoba mwaka huu ambayo yatajumuisha washiriki kutoka mikoa yote hapa nchini.

Mapema, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi hapa nchini (ILO Tanzania), Bw. Alexio Musindo, alisema anawapongeza akinamama wajasiriamali chini ya kamati ya MOWE kwani kupitia mafunzo yanayodhaminiwa na Ofisi yake, akianamama hao wameweza kujiamini zaidi na kuthubutu kushiriki maonyesho mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema jamii haina budi kuwekeza zaidi kwa wasichana kwa kuwapa fursa za kujiendesha kibiashara pamoja na ujuzi (skills) ili waweze kujiajiri kwani wanakumbana na vikwazo vingi wanapotafuta ajira ikiwemo, unyanyasaji na unyanyapaa.









All the contents on this site are copyrighted ©.