Wanahabari zaidi ya 5,600 wako Mjini Vatican ili kutoa taarifa juu ya mchakato wa
uchaguzi wa Papa Mpya!
Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kwa kushirikiana na Radio Vatican, Kituo
cha Televisheni cha Vatican na Idara ya Habari ya Vatican katika ujumla wake, wameanzisha
kituo maalum cha huduma za mawasiliano ya Jamii, ili kuwawezesha waandishi wa habari
5,600 kutoka sehemu mbali mbali za dunia kupata habari za uhakika kuhusu mchakato
wa uchaguzi wa Papa Mpya unaoendelea hapa mjini Vatican.
Baraza la Kipapa la
Mawasiliano ya Jamii linabainisha kwamba, lina uzoefu wa kutosha kufuatia kifo cha
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili sanjari na kutangazwa kwake na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, kuwa Mwenyeheri, ni kati ya matukio ambayo yaliwakusanya
waandishi wa habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakaridhika na huduma iliyokuwa
inatolewa. Kituo hiki cha habari wakati huu wa mchakato wa kumchagua Papa Mpya kimewekwa
kwenye Ukumbi wa Paulo wa VI, unaoweza kutoa huduma kwa waandishi wa habari, watangazaji
wa Radio na Televisheni pamoja na wapiga picha za kawaida.
Waandishi wa habari
waliosajiliwa kwa wakati huu ni kutoka katika nchi 65 wanaowakilisha lugha 24 za kitaifa
na kimataifa. Baadhi ya vyombo hivi vya habari vinawasindikiza Makardinali kutoka
katika nchi zao, kila chombo kikiwa na lengo lake maalum. Radio Vatican inaendelea
kutoa huduma kwa vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya Jamii kwa ufanisi mkubwa. Kuna
jumla ya vyumba 15 vilivyotengwa maalum kwa ajili ya watangazaji wa radio.
Hadi
sasa kuna zaidi ya radio 55 zinazojiunga moja kwa moja na Radio Vatican ili kupata
habari za uhakika kutoka hapa mjini Vatican. Vituo vingi vya Radio vinatumia sauti
inayotolewa na Radio Vatican pamoja na picha zinazorushwa na Kituo cha Televisheni
cha Vatican.