Waamini wanasali ili kuombea mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya
Makardinali wanaohudhuria mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro hapa mjini
Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe 10 Machi 2013 wameungana na waamini wa Parokia
zao za kitume walizokabidhiwa walipokuwa wanasimikwa kuwa Makardinali, kielelezo cha
mshikamano na umoja na Askofu wa Jimbo kuu la Roma. Ibada hizi zimehudhuriwa pia na
waamini kutoka katika nchi husika.
Lengo ni kuwawezesha Makardinali katika
kipindi hiki maalum cha maisha na utume wa Kanisa kutafakari na kusali kwa ajili ya
kuombea ufanisi katika uchaguzi wa Papa Mpya ambao unaanza rasmi tarehe 12 Machi 2013.
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu lililofanyika kwenye Parokia
ya Bikira Maria wa Salette alisema kwamba, ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa sasa
na kwa siku za usoni, umedhaminishwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Makardinali
kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekusanyika mjini Roma kuanza mchakato wa kumchagua
Khalifa wa Mtakatifu Petro, utume ambao Mwenyezi Mungu anawakabidhi binadamu, akitumaini
kwamba, neema yake itawasaidia kutekeleza wajibu huu msingi, ili Mungu aweze kupata
makao miongoni mwa binadamu anayepaswa kuwa kweli ni mdau mkuu katika utekelezaji
wa mipango ya Mungu katika kazi ya ukombozi.
Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili
wa Kristo, linashirikiana kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Khalifa
wa Mtakatifu Petro anayo dhamana kubwa ya kuwaongoza Watu wa Mungu kutekeleza wito
wao, kwa kutambua nafasi na fursa walizokirimiwa katika kuendeleza historia ya ukombozi
wa mwanadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo ambaye kimsingi ni daraja
kati ya Mungu na mwanadamu.
Kardinali Peter Erdo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya katika maadhimisho ya Ibada ya Ekaristi Takatifu,
Jumapili iliyopita, ameendelea kuwaalika waamini kuisikiliza sauti ya Kristo, mchungaji
mkuu, wawe tayari kutubu na kumwongokea Mungu, kama alivyofanya yule Mwana Mpotevu,
ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Ni changamoto na mwaliko kwa
waamini kuendelea kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yao adili, ili walimwengu
waweze kumwamini Kristo.
Kwa upande wake, Kardinali Angelo Scola wa Jimbo kuu
la Milani, amewataka waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulijalia Kanisa kiongozi
makini atakayefuata nyayo za watangulizi wake, yapata miaka 150 iliyopita!.