Uhuru Kenyatta (51) akata mzizi wa fitina nchini Kenya!
Tume huru ya uchaguzi na mipaka imemtangaza Bwana Uhuru Kenyatta (51) kuwa Rais mpya
wa Kenya baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi
2013 kwa kumshinda mpinzani wake wa karibu Bwana Raila Odinga. Baada ya kutangaza
matokeo ya Urais, Mahakama kuu ina siku 14 za kisheria za kutoa uamuzi juu ya pingamizi
lolote dhidi ya matokeo ya urais.
Watu kutoka ndani na nje ya Kenya wanaendelea
kuwapongeza wananchi wa Kenya kwa kufanikisha uchaguzi kwa amani na utulivu. Wakati
wa Kampeni na hatimaye, uchaguzi wenyewe, viongozi wameonesha ukomavu wa kisiasa kwa
kutoa kwanza kabisa kipaumbele kwa mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Kenya. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyingine Barani Afrika.
Mwenyekiti
wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka anawapongeza wananchi wa Kenya, vyombo vya habari
kwa kufanikisha uchaguzi kwa asilimi 86%, hali ambayo imefikiwa kwa mara ya kwanza
nchini Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anawashukuru wananchi kwa kumpatia
kura ambazo zinamwezesha sasa kuongoza nchi na kutekeleza yale ambayo wameyabainisha
katika Ilani ya uchaguzi wa Chama chake. Anaahidi kuwatumikia Wakenya wote katika
hali ya usawa sanjari na kuendeleza gurudumu la maendeleo kwa Wakenya wote. Ni matumaini
ya Rais Kenyatta kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaheshimu maamuzi ya wananchi wa Kenya
waliyoyafanya kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Bwana Raila Odinga anawashukuru
wananchi wa Kenya kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu.
Anasema ana imani na vyombo vya sheria nchini Kenya, kumbe, atapinga matokeo ya uchaguzi
mkuu Mahakamani.
Itakumbukwa kwamba, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anakabiliwa
na mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, kama ilivyo pia
kwa Mgombea mwenza Bwana William Ruto (46). Wanashutumiwa kwa kusababisha machafuko
ya kisiasa yaliyopelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao mara baada ya matokeo ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 kutangazwa.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alizaliwa
kunako tarehe 26 Oktoba 1961. Ni mtoto wa Rais Mzee Jomo Kenyatta na Mama Ngina Kenyatta.
Tangu mwaka 2008 alikuwa ni Makamu wa Waziri mkuu wa Kenya. Tangu mwaka 2003 alikuwa
ni Mbunge wa Jimbo la Gatundu Kusini. Kunako mwaka 2002 aliteuliwa na Rais Daniel
Arap Moi kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya KANU, akashindwa katika uchaguzi na Rais
Mwai Kibaki. Ni Mwanasiasa Kijana ambaye anashikamana na kijana mwenzake katika kuwaongoza
wananchi wa Kenya!