Makardinali wako tayari kwa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumanne tarehe 12 Machi 2013, saa
4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, itakayohudhuriwa na Makardinali pamoja
na Familia ya Mungu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Mkutano
wa Makardinali umeamua kwamba, Kikao cha uchaguzi wa Papa Mpya kitaanza rasmi Jumanne,
tarehe 12 Machi 2013. Majira ya saa 10:30 Jioni kwa saa za Ulaya, Makardinali wataingia
kwenye Kikanisa cha Paulo, tayari kuingia kwenye Kikanisa cha Sistina, wakiongozwa
na nyimbo za kuomba mapaji ya Roho Roho Mtakatifu wanapoanza kutekeleza dhamana hii
nyeti kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo.
Kikao hiki kitaanza
kwa Makardinali kula kiapo cha siri kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa. Conclave
inapoanza, lango linafungwa na hapo waamini wanaendelea kuwasindikiza Makardinali
kwa njia ya sala, wakisubiri kuona moshi mweupe alama kwamba, Kanisa limempata Papa
Mpya!
Wakati huo huo, Maafisa na wote watakaohusika na shughuli za Conclave,
tarehe 11 Machi 2013, majira ya jioni wanakula kiapo cha kutunza siri za uchaguzi
wa Papa Mpya kama ilivyoamriwa na sheria pamoja na kanuni za Kanisa. Ibada ya kula
kiapo itafanyika kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo.
Hawa ni Katibu wa Makardinali,
Washereheshaji wa Ibada za Kipapa, Mapadre walioteuliwa kwa kazi maalum, Watawa wanaohudumia
Sakristia, Madaktari na wauguzi, wafanyakazi wanaolinda usalama, wahudumu na wataalam.
Kundi hili litajulishwa umuhimu wa tukio hili kwa maisha na utume wa Kanisa. Wataandika
na kutamka wazi kiapo hiki mbele ya Kardinali Camerlengo, Tarcisio Bertone pamoja
na mawakili wawili ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka.
Padre Federico
Lombardi akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma, amefafanua kwamba,
Makardinali wataanza kuingia kwenye vyumba walivyopangiwa kwenye Hosteli ya Sanctae
Marthae iliyoko ndani ya mji wa Vatican, tarehe 12 Machi 2013, kuanzia saa 1:00 na
kuendelea, ili kuwapatia nafasi ya kujiandaa kwa ajili ya kushiriki katika Ibada ya
Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hapo saa
4:00 asubuhi.
Mkutano wa Makardinali unaendelea hata Jumatatu, ili kutoa nafasi
kwa Makardinali ambao walikuwa bado hawajashirikisha mawazo yao kuzungumza kabla ya
kuanza rasmi mchakato wa kumchagua Papa Mpya. Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV
kitarusha picha maalum katika matukio haya maalum wakati wahudumu wa Conclave wa kula
kiapo kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya.