2013-03-11 08:16:45

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zake nchini Japan


Baraza la Maaskofu Katoliki Japani katika ujumbe wake wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani wanasema, ni mwaliko na changamoto kwa kila mwamini kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kwa Familia ya Mungu nchini Japan, ina changamoto nyingi zaidi. RealAudioMP3

Ni mwaliko kwa waamini nchini Japani kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, kwa kufanya tafanari ya kina kuhusu damu ya mashahidi wa Japan, ambao ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani yao. Kanisa halina budi kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na changamoto hizi kwa sasa na kwa siku zijazo, kwa kuhakikisha kwamba, waamini wanaifahamu kwa kina Imani inayoungamwa, adhimishwa, mwilishwa na kusaliwa mintarafu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, ambayo inatimiza miaka ishirini tangu ilipochapishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, bado waamini wengi hawajaifahamu imani yao, kiasi hata cha kushindwa kuitolea ushuhuda katika maisha ya hadhara.

Maaskofu Katoliki Japan wanaalikwa waamini kujikita zaidi katika azma ya Uinjilishaji Mpya kadiri ya mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambao unautajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Ni Mtaguso ambao umeleta chachu ya mabadiliko na mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki katika medani mbali mbali za maisha na utume wake; katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, hii ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, tayari waamini kujitosa kimaso maso kufanya toba na wongofu wa ndani.

Mwaka wa Imani nchini Japan unakwenda sanjari na Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 150 tangu Wafia dini ishirini na sita walipotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Watakatifu, changamoto na mwaliko wa kuchuchumilia wito na dhamana ya dimissionari. Maaskofu wanawaalika waamini kuwakumbuka hata wale ambao miaka mia nne na kumi na tano iliyopita, waliyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alipotembelea Japan kunako mwaka 1981, aliwaambia waamini kwamba, Kanisa nchini Japan limesimikwa katika msingi wa damu ya mashahidi na wafiadini. Hii ndiyo istoria ya ajabu ambayo Mwenyezi Mungu amependa kwa busara yake wanasema Maaskofu kuwaandalia waamini nchini Japan, kama njia ya wokovu. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anaendelea kulihamasisha Kanisa kujikita katika Uinjilishaji Mpya, kwa kusoma, na kulitafakari Neno la Mungu; kwa njia ya Sala na Maisha ya Kisakramenti pamoja na kuwashirikisha wengine .

Japan inakabiliana na changamoto kubwa katika kulinda na kutunza mazingira baadaya maafa makubwa yaliyoikumba nchi hii hivi karibuni; kuna athari kubwa za myumbo wa uchumi kimataifa; idadi ya watoto ya watoto wanaozaliwa nchini Japan imeshuka kwa kiwango kikubwa, kiasi cha kutishia usalama na ustawi wa nchi kwa siku za usoni, kwani kuna idadi kubwa ya wazee wanaohitaji kupata huduma kwa njia ya hifadhi za kijamii.

Kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kuna ongezeko kubwa la watu wanaotema zawadi ya maisha kwa njia ya kujinyonga wenyewe, kumeibuka uhusiano tenge katika mahusiano ndani ya jamii, bila kusahau hatari kubwa iliyoko mbele ya wananchi wa Japan kutokana na Mambo wa kuzalisha nguvu za Kinyuklia. Yote haya ni matokeo ya sera na mawazo tenge, ambayo yamepelekea watu wengi kuanza kujiuliza nini maana ya maisha na wokovu wa binadamu?

Maaskofu katoliki nchini Japan wanawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, wao wamebahatika kupokea zawadi ya Imani, ambayo wanapaswa kuitolea ushuhuda makini, kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya patendo yao adili, wakionesha kwamba, wanaandamana na Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Hiki ni kipindi cha kufurahia zawadi ya Imani ambayo ni chemchemi ya fadhila ya Matumaini.

Maafa yaliyojitokeza nchini Japan tarehe 11 Machi 2011, baada ya mtambo wa Fukushima Daiichi kuvuja na hivyo, kupelekea maelfu ya watu kupoteza maisha, wengi wakayakimbia na kuyahama makazi yao kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu, kwa hakika lilikuwa ni tukio la kukatisha tamaa. Hii ni nafasi ya kufanya tafanari ya kina, jinsi ya kuishi na kushuhudia Imani katika matukio kama haya katika historia.

Inatia moyo kuona jinsi ambavyo waamini kutoka sehemu mbali mbali nchini Japan walivyojifunga kibwebwe kuwasaidia waliokuwa wameathirika kutokana na maafa yale, ili kuanza tena upya hija ya maisha yao hapa duniani, kwa imani na matumaini mapya. Wahanga wa maafa yale, wamekuwa ni fundisho na msaada mkubwa kwa wote waliojitaabisha kwenda kuwasaidia, kwani waliporudi makwao walijikuta wakiwa wamebeba utajiri mkubwa katika maisha yao ya kiroho, ni watu ambao licha ya maafa yale, bado wameendelea kuwa na matumaini, huu ni mwanga mpya wa Imani kwa wananchi wa Japan.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japani mwishoni mwa barua yao ya kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani wanabainisha kwamba, Familia ya Watu wa Mungu nchini Japan iko katika hija, inayowaelekeza katika mlango wa Imani; kwa unyenyekevu na ujasiri mkubwa, wanaalikwa kusikiliza sauti ya wale wanaoteseka na kuwasaidia kadiri ya uwezo wao, kama njia ya ushuhuda unaopania kukoleza moyo wa Uinjilishaji Mpya, kwa wale walioko ndani ya Kanisa na wale ambao bado hawajabahatika kuuona mlango wa Imani.








All the contents on this site are copyrighted ©.