Umaarufu wa Kikanisa cha Sistina wakati wa chaguzi za Mapapa
Kikanisa cha Sistina kimefanyiwa marekebisho ili kuweza kutoa fursa kwa Makardinali
kutekeleza wajibu na dhamana nyeti ya kumchagua Baba Mtakatifu Mpya, baada ya Papa
Benedikto wa kumi na sita, kwa utashi na uhuru kamili kuamua kung’atuka kutoka madarakani
hapo tarehe 28 Februari 2013. Hii itakuwa ni
mara ya ishirini na tano kwa uchaguzi wa Papa kufanywa ndani ya Kikanisa cha Sistina
chenye utajiri mkubwa wa sanaa. Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya,
Kikanisa cha Sistina kitakuwa kimefungwa kwa watalii na mahujaji kutoka sehemu mbali
mbali za dunia wanaofika mjini Vatican kushangaa maajabu ya Mungu yaliyotendwa kwa
mikono ya wanadamu! Kunako Mwaka 1996 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika
Waraka wake wa Kichungaji kuhusu uchaguzi wa Papa, unaojulikana kama “Universi Dominici
Gregis” aliamua kwamba, tangu wakati huo, uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro,
utakuwa unafayikia ndani ya Kikanisa cha Sistina, ambacho kwa Mwaka 2013 kitatoa nafasi
kwa Makardinali 115 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura kushiriki katika uchaguzi
wa Papa Mpya. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 1939 Kikao cha Makardinali kilichomchagua
Papa Pio wa kumi na mbili, kilianza kutumia kwa mara ya kwanza Jiko ambalo linatumika
kwa ajili ya kuchoma kura za Makardinali wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya. Hapa ndipo
ilipolala siri ya moshi mweupe unaosubiriwa kwa hamu kubwa na waamini kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, ambao wanaendelea kufuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya
mawasiliano ya Jamii.