Mkusanyiko wa Mahubiri ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI siku chache kabla ya kung'atuka
kutoka madarakani zimechapishwa katika kitabu!
Idara ya uchapaji ya Vatican imechapisha kitabu ambacho kinajulikana kwa jina "I Have
Never Felt Alone" "Sijawahi Kamwe Kujisikia Upweke", maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita wakati wa Katekesi aliyoitoa hapo tarehe 27 Februari 2013, Siku moja
kabla ya kung'atuka kutoka madarakani.
Ni kitabu kinachoonesha maneno ambayo
yatabakia kuwa ni wosia wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kabla ya kutoweka
katika maisha ya hadhara, ili kupanda kwenda Mlimani kusali na kufanya tafakari ya
kina. Hii siku ambayo umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia ulimiminika
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuonesha upendo na
mshikamano kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyeliongoza Kanisa kwa
imani, busara na hekima kubwa katika kipindi chote cha miaka minane ya uongozi wake
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Nyuma ya Kitabu kumeandikwa maneno ya Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo,
aliposema kwamba, sasa yeye ni hujaji wa kawaida anayeanza hatua ya mwisho ya maisha
yake hapa duniani. Huu ni mchango wa Idara ya Uchapaji ya Vatican kwa kutambua na
kuthamini utume wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ambaye ameridhia mwenyewe
kutoa utangulizi wa kitabu hiki.
Idara ya Uchapaji ya Vatican imekuwa bega
kwa bega na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika maisha na utume wake kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, ameitumia idara hii kama chombo cha kutangaza
Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Kitabu kina hotuba ya Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, aliyoitoa kwa Makardinali hapo tarehe 11 Februari 2013
akionesha utashi na uhuru kamili wa kung'atuka kutoka madarakani ifikapo tarehe 28
Februari 2013. Kuna Katekesi ya kina, ambayo kimsingi ni muhtasari wa utume wake kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyoitoa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
Jumatano ya Majibu, jioni aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro na kutoa mahubiri ambayo yanaendelea kutoa mwangwi katika maisha na utume wa
Kanisa. Tarehe 28 Februari 2013, Baba Mtakatifu alizungumza na Makardinali, hotuba
ambayo pia iko kwenye Kitabu hiki.
Idara ya uchapaji ya vatican inafafanua
kwamba, kitabu hiki kina waraka wa kichungaji kuhusu mabadiliko ya uchaguzi wa Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Kwa sasa kinatolewa katika lugha ya Kiitalia.