2013-03-09 10:34:44

Matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Kenya


Uhuru Kenyata ameshinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013 kwa asilimia 50.3% dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga aliyepata asilimia 43.3%. Hata hivyo Raila Odinga ameonesha nia ya kutaka kukata rufaa mahakama kuu ili kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Kenya ambayo anasema kwamba, yaligubikwa na uganganyifu mkubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake mara baada ya uchaguzi mkuu, linaendelea kuwataka wananchi wa Kenya kudumisha amani na utulivu. Wanawashukuru na kuwapongeza wanasiasa ambao wamekubali kwamba, wameshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba, kwa sasa wanaendelea kudumisha amani. Kwa wale ambao hawataridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu, wanasema Maaskofu wana haki ya kukata rufaa mahakamani pamoja na kuendelea kuwahimiza mashabiki wao kuwa watulivu.

Maaskofu Katoliki Kenya wanawataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za kila siku katika ujenzi wa nchi; wanafunzi warudi shuleni na vyombo vya usafiri vitekeleze wajibu wake barabara. Maaskofu wanawashukuru wananchi wa Kenya kwa kudumisha amani na utulivu hata kama kuna baadhi ya sehemu zimetikisika kidogo kwa watu kupoteza maisha yao.

Barua ya Baraza la Maaskofu Kenya imetiwa mkwaju na Askofu Philip Anyolo, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa niaba ya Maaskofu wenzake.







All the contents on this site are copyrighted ©.