Makardinali 115 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura kumchagua Papa wa 266 wako tayari
mjini Vatican
Mkutano wa nane wa Makardinali uliofanyika Ijumaa tarehe 8 Machi 2013 umewashirikisha
Makardinali 153, kati yao Makardinali 115 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura. Kardinali
Angelo Sodano Dekano wa Makardinali ndiye aliyeongoza mkutano huo, kwa kufafanua baadhi
ya vipengele vya Waraka unaohusu uchaguzi wa Papa Mpya, unaowaruhusu kuanza mkutano
rasmi baada Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura wanapokuwa wamewasili
wote, ikiwa kama hakuna pingamizi au sababu za msingi.
Lakini imefafanuliwa
kwamba, zinapopita siku 20 tangu Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kilipoachwa wazi,
Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura wanalazimika kuanza mchakato
mara moja kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa.
Mchakato wa uchaguzi wa Khalifa
wa Mtakatifu Petro ni tukio ambalo linafuatiliwa na mamillioni ya watu anasema Padre
Federico Lombardi. Makardinali wameanzisha mshikamano wa sala na waamini kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, ambao kwa sasa idadi yao ni zaidi ya watu 220, 000, wanaojitoa
kwa ajili ya kuwaombea Makardinali katika kipindi hiki wanapojiandaa kwa ajili ya
uchaguzi wa Papa Mpya. Kikao cha Conclave kinaanza rasmi Jumanne, tarehe 12 Machi
2013 kwa Ibada ya Misa Takatifu.
Kati ya mambo yanayoendelea kupewa msukumo
wa pekee katika mkutano wa Makardinali ni pamoja na majadiliano ya kidini, kiekumene
na kitamaduni; maadili, haki na amani katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Wamekazia tasahufi ya huruma na upendo katika maisha na
utume wa Kanisa, kwa kuendelea kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu
wanapotekeleza wajibu na dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu
wa Mungu.
Makardinali pia wamejadili kuhusu dhamana na mchango wa wanawake
katika maisha na utume wa Kanisa. Katika mkutano wa Makardinali, kila Kardinali amepewa
nafasi ya kuzungumza mara moja, ili kutoa nafasi kwa Makardinali wengine pia kushirikisha
mang'amuzi yao mintarafu utume wa Kanisa la Kiulimwengu.
Padre Lombardi anasema
kwamba, Domus Santae Marthae itatumika kama makazi kwa Makardinali wakati wote wa
uchaguzi. Mpango na mgawanyo wa vyumba unafanywa na Makardinali wenyewe kwa njia ya
bahati nasibu na hakuna Kardinali anayechagua nani aweze kuwa jirani yake au angependelea
kuishi katika chumba gani! Papa Mpya atakayechaguliwa kwenye Mkutano wa Makardinali,
atalazimika kuishi kwa muda kwenye Hosteli hii, wakati ambapo Jengo la Kitume litakapokuwa
limefunguliwa na ukarabati mdogo kufanyika.
Padre Federico Lombardi anabainisha
kwamba, licha ya ukweli kuwa Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi, lakini Mabaraza
ya Kipapa yanaendelea na shughuli zake za kawaida. Kardinali Prospero Grech anatarajiwa
kutoa tafakari kwa Makardinali wakati wa mkutano wao.