2013-03-09 09:44:39

Majiundo makini ya Makleri ndani ya Kanisa


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alifanya marekebisho makubwa katika Sheria na Katiba ya Kitume Pastor Bonus, iliyokuwa imetolewa na Papa Yohane Paulo wa Pili, kunako mwaka 1988. RealAudioMP3
Waraka huu mpya unaojulikana kama Ministrorum Institutio uliotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita unahamisha: dhamana na madaraka ya Seminari kutoka katika Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na kuyapeleka katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri.
Baba Mtakatifu anasema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walionesha umuhimu wa Mama Kanisa kujikita katika majiundo makini ya Makleri mintarafu Sheria na Kanuni za Kanisa, ili hatimaye, waweze kutekeleza wajibu wa kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu.
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Seminari likapewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, Waseminari wanapata majiundo makini kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa Nane, katika Waraka wake wa Creditae Nobis wa Mwaka 1725. Kanisa likaendelea kutoa kipaumbele kwa majiundo ya waseminari kwa kufanya marekebisho mbali mbali yanayojionesha kwa namna ya pekee katika Sheria za Kanisa za Mwaka 1917.
Katika Muswada wa Sheria Mpya za Kanisa, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, iliamriwa kwamba, maelezo kuhusu majiundo ya Waseminari yawe ni sehemu ya utangulizi kuhusu sheria na kanuni za Kanisa kuhusiana na wito wa Upadre. Hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa hatua mbali mbali za malezya maisha na wito na Kipadre.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji, Pastor Dabo Vobis wa Mwaka 1992 anakazia umuhimu wa kutambua na kuheshimu uhusiano uliopo kati ya majiundo makini kabla ya kupewa Daraja Takatifu, wakati wa kupewa sanjari na Majiundo endelevu ya Kipadre. Lengo ni kuendeleza mshikamano wa upendo na utume miongoni mwa Mapadre wenye umri tofauti.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, ni kutokana na sababu hizi msingi kuhusu majiundo na malezi ya kipadre; maisha na utume wa Mapadre na Mashemasi, ameamua kuhamishia dhamana na utume huu katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri. Baraza hili litakuwa na dhamana ya kuhamasisha, kutunza na kuchagua wale wanaofaa kwa ajili ya maisha na wito wa Kipadre.
Baraza ltajikita pia katika maisha ya mtu mzima: kiutu, kiroho, kielimu na kuainisha mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa katika Seminari na Nyumba za Malezi na Majiundo ya Kipadre. Litashughulikia pia majiundo endelevu ya Mapadre na Mashemasi wa kudumu, ili kuwawezesha kutekeleza kwa umakini mkubwa utume wao pamoja na kuzingatia masilahi yao ya kijamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.