2013-03-09 08:20:47

Conclave: ni kipindi cha imani, sala na matumaini


Askofu mkuu Juan Ignacio Arrieta, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la sheria anabainisha kwamba, wakati ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi, shughuli msingi za Kanisa zinaendeshwa na Dekania ya Makardinali, lakini kwa maneno machache ni shughuli zinazoensdeshwa mintarafu sheria na kanuni za Kanisa. RealAudioMP3

Katika kipindi hiki, Mabaraza ya Kipapa yanawajibika kutekeleza majukumu yake ya kawaida, kwani kimsingi anapong’atuka kutoka madarakani kama ilivyokuwa kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Marais na Wenyeviti wa Mabaraza ya Kipapa nyadhifa zao zinakoma kisheria, kwani kadiri ya sheria za Kanisa wanakosa rejea na maamuzi ya mwisho yanayopaswa kutolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kwa vile matukio kama haya yanakuja kwa nadra sana, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuvya taratibu ili uweze kufahamu walau mambo ya msingi yanayoendelea ndani ya Kanisa kwa wakati huu Makardinali wanapoendelea na mikutano yao kama sehemu ya mchakato wa kumchagua Papa Mpya wakati utakapowadia.

Con-clave: neno ambalo litasikika sana wakati huu wa mchakato wa kumchagua Papa Mpya linatoholewa kutoka katika Lugha ya Kilatini, maana yake, “Kufunga na ufunguo”. Wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya, Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura hujifungia kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican.

Hiki ni kile kipindi kilichokubalika katika kukuza na kuimarisha misingi ya imani, matumaini na mapendo ya kidugu miongoni mwa Familia ya Mungu; lakini kwa namna ya pekee kwa Makardinali waliokabidhiwa dhamana ya kushiriki katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha imani, matumaini, mapendo, umoja na mshikamano wa Kanisa.

Uchaguzi wa Papa wakati huu unafanyika katika Kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Haya ni matukio yenye utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanakumbushwa kwamba, hata kama Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ameng’atuka kutoka madarakani, lakini Kristo bado anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu na kamwe haliwezi kuwa ni yatima!

Ni mwaliko kwa waamini kuyaangalia matukio yote haya kwa jicho la imani na matumaini mintarafu mpango wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Askofu mkuu Juan Ignacio Arrieta anasema kwamba, mikutano ya Makardinali iliyoanza tangu Jumatatu tarehe 4 Machi 2013 inawajumuisha Makardinali wote bila kutofautisha wale wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura. Kimsingi ni mkutano ambao unajadili namna ya kufanya maziko ya Papa.

Ikumbukwe kwamba, tukio la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kung’atuka kutoka madarakani linafanyika takribani baada ya miaka 600 ya historia ya Kanisa Katoliki, ndiyo maana watu wengi wamepigwa na bumbuwazi. Kumbe, ni Makardinali waliokuwa na dhamana ya kusoma Wosia wa Papa aliyefariki dunia na hivyo wanakuwa na dhamana pia ya kupanga siku ambayo wataanza mchakato rasmi wa uchaguzi wa Papa Mpya. Hapa neno Conclave, yaani “Con Chiave” kwa lugha ya Kiitalia; Waswahili wakatafsiri kwa kusema “kufunga na ufunguo” linapata umuhimu wa pekee.

Ni Makardinali peke yao wanaoruhusiwa kuhudhuria mikutano hii kwani hapa wanalichambua Kanisa “kama karanga” ili kubainisha hali ya Kanisa, matatizo yaliyopo, fursa na changamoto ambazo wanapaswa kuzifanyia kazi kwa siku za usoni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Kutokana na mwelekeo kama huu, hapa Makardinali wanaanza kupata walau “fununu” ya Papa anayetarajiwa na Mama Kanisa.

Conclave, neno ambalo tutaendelea kulitumia jinsi lilivyo ni kipindi cha sala. Ndiyo maana Makardinali kila siku jioni wanakutanika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kusali, kutafakari na kuabudu Ekaristi Takatifu. Sehemu hii inaongozwa na Sheria za Kanisa kuhusu Liturujia, ili waweze kuongozwa na Roho Mtakatifu katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Lengo ni kuwapatia Makardinali fursa ya kuweza kusali na kutafakari bila kuwa na haraka, kwani mambo mazuri hayataki haraka ndivyo wanavyojutuza Waswahili. Ni kipindi ambacho Makardinali wanajiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza bila kushinikizwa na watu au sera za makundi ya kijamii.

Papa anayechaguliwa kimsingi ni mtu ambaye anatarajiwa kuweza kukabiliana na changamoto za Kanisa kwa wakati wake, kama inavyojionesha pia katika kiapo na kura wanazopiga. Kura zinapigwa mara mbili: ya kwanza inapigwa asubuhi na kura ya pili inarudiwa jioni, ili kuwapatia Makardinali mwelekeo wa kuamua ni yupi kati ya wale ambao wamependekezwa anayeweza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kuliongoza Kanisa.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako mwaka 2007 aliamua kwamba, ili Kardinali aweze kuchaguliwa kuwa Papa lazima apate theluthi tatu ya kura zote halali na kwamba, Conclave inaweza kufanyika mapema kadiri ya maamuzi ya Makardinali kwa kusoma alama za nyakati na hivi ndivyo itakavyokuwa.

Sheria na kanuni zinazoongoza uchaguzi wa Papa Mpya ni nyeti na adhabu yake ni kujitenga na Kanisa mara moja pasipo na huruma yaani kwa lugha ya sheria za Kanisa hali kama hii inajulikana kama “Latae Sententiae”. Lengo ni kulinda uhuru wa Makardinali katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni mwelekeo wa maisha ya kiroho unaooneshwa wakati wa Conclave. Hapa hakuna ushawishi kutoka nje, kama inavyojionesha kwa sasa, kila upande ukiwapigia “debe” Makardinali wanaodhani kwamba, wanaweza kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ikumbukwe kwamba, kwa Kardinali kuchaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni dhamana nyeti inayogusa utume wake. Huu si “ujiko” au fahari ya mtu. Hivi karibuni kumekuwepo na kampeni kubwa iliyofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwachafua watu pamoja na kuwawekea vizingiti kiasi kwamba, hawataweza kushiriki katika uchaguzi wa Papa Mpya. Hapa waamini wakumbuke kwamba, huu si uchaguzi wa kisiasa kama wengi walivyozoea.

Kanisa anasema Askofu mkuu Juan Ignacio Arrieta, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa kwamba, lina imani na Roho Mtakatifu anatakayewawezesha Makardinali kufanya maamuzi ya busara pasipokuwa na shinikizo kutoka sehemu yoyote ile!

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.