Wanawake simameni kidete: kutetea, kulinda na kueneza Imani kwa Kristo Mfufuka kwa
njia ya maisha yenu adili!
Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anabainisha kwamba, Wanawake Wakatoliki wanayo fursa kubwa ya kuboresha,
kuimarisha pamoja na kurithisha imani kwa Kanisa mahalia.
Jambo la msingi
ni kuhakikisha kwamba, wanawake wanakuwa mstari wa mbele: kutetea, kulinda na kuineza
imani ya Kristo mfufuka, kama walivyofanya wale wanawake watakatifu wanaosimuliwa
kwenye Maandiko Matakatifu.
Ni wanawake waliomsindikiza Yesu katika Njia yake
ya Msalaba, wakadiriki kusimama chini ya Msalaba, wakataza mahali alipozikwa, alfajiri
na mapema wakaenda kutaka kuutengeneza mwili wake. Ni wanawake hawa watakatifu waliopewa
dhamana ya kutangaza ufufuko wa Kristo, pale waliposhuhudia kwa nguvu kwamba, "Kaburi
li wazi". Yesu katika maisha na utume wake, aliinua utu na heshima ya wanawake waliokuwa
wanadharauliwa katika Jamii kwa wakati ule.
Mfumo dume hata katika Jamii nyingi
za Kiafrika bado hautowi nafasi kwa wanawake wengi kushiriki kikamilifu katika maisha
ya kijamii hata pengine katika utume wa Kanisa. Kuna haja kwa wanawake kujiamini na
kwamba, maadhimisho ya Miaka 40 ya Chama Cha Wanawake Wakatoliki Tanzania, yaliyofanyika
hapo mwaka 2012 iwe ni chachu ya kuzaa matunda yanayokubalika, kwa kujikita katika
toba na wongofu wa ndani; kwa kutambua na kuthamini ushiriki wao katika kutunza, kutetea
na kurithisha imani.
Wanawake hawana budi kuwezeshwa kikamilifu ili waweze
kutekeleza utume na dhamana yao kwa Jamii na Kanisa, vinginevyo, Kanisa litaendelea
kuchechemea katika kueneza imani, maadili na utu wema, kwani wanawake wanayo nafasi
ya pekee kabisa katika utekelezaji wa dhamana hii.
Askofu Michael Msonganzila
anabainisha kwamba, kutokana na ukata na hali ngumu ya uchumi, uwepo wa familia tenge
na majukumu makubwa wanayowakabili wanawake wengi; vyama vingi vya kisiasa na uelewa
tenge wa demokrasia umepelekea wanawake wengi kujikuta wakimezwa na malimwengu. Ikumbukwe
kwamba, wakati wa migogoro ya kivita na kijamii, waathirika wakubwa ni wanawake na
watoto.
Ni wajibu wa wanawake kusimama kidete kukemea na kulaani vitendo vyote
vinavyopelekea kinzani, migogoro na nyanyaso, kwani kila mtu anachangamotishwa kuwa
ni mjenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli. Ukimwi bado ni
janga kubwa kwa Jamii nyingi za Kiafrika na waathirika wakubwa anasema Askofu Msonganzila
bado ni wanawake.
Ni changamoto kwa wanawake kusimamia maadili na utu wema,
wasikubali kutumbukizwa katika utumwa wa ngono na biashara haramu ya binadamu; mambo
ambayo yananyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya wanawake na wasichana.
Wanawake
wanapaswa kujifunga kibwebwe kuboresha maisha yao kwa njia halali na wasikubali njia
za mkato kwani zinaweza kuwatumbukiza katika madhara makubwa zaidi hata pengine kwa
gharama ya maisha na familia zao. Wanawake wapambane kufa na kupona pale inapowezekana
ili waweze kujikomboa kiuchumi, kijamii pamoja na kuimarika kiimani. Watambue daima
kwamba, hakuna njia ya mkato katika maisha! Kila mtu awajibike kutafuta maisha bora
zaidi kwa njia halali!