Wanawake ni walezi wa kwanza katika Jamii, changamoto ya kutekeleza wajibu wao!
Bi Imelda Kalolo kutoka Dodoma, Tanzania, katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha
kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna
haja kwa wanawake kusimama kidete katika misingi ya imani, maadili na utu wema kwa
njia ya mifano bora ya maneno lakini zaidi kwa maisha adili na matakatifu.
Wanawake wajitahidi
kuwa wachamungu kwa njia ya sala, ili kweli waweze kuwa ni chachu ya utakatifu na
maisha adili miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, wanawake kimsingi
ni walimu wa kwanza wa maisha ya sala na adili kwa watoto wao! Kutokana na mfumo wa
maisha kuendelea kubadilika kwa kasi, vijana wengi wanajikuta wanamezwa na malimwengu,
kiasi cha kupotoka na kukengeuka!
Hili Jamii iweze kuwa na vijana wenye msingi
bora wa maisha adili yanayokubalika mbele ya Mungu na Jamii, kuna haja kwa wanawake
kujifunga kibwebwe ili waweze kuwa kweli ni mifano bora ya kuigwa, kwa kutekeleza
wajibu wao wa kwanza ambao ni malezi kwa watoto wao! Wazazi wenyewe wawe ni watu wenye
msingi bora wa maadili na thabiti katika imani inayojionesha katika matendo. Wasaidie
kukoleza miito mitakatifu katika Kanisa kwa kutambua kwamba, Mapadre na Watawa wema
na watakatifu wanatokana na Familia bora za Kikristo.