2013-03-08 07:43:06

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima: Baba mwenye huruma!


Tunaendelea na tafakari Neno la Mungu Dominika ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima mwaka C na Injili ya Bwana yatufundisha mapendo ya Mungu kwa watu wake wote bila kujali nani ana dhambi na nani ni mwema. RealAudioMP3

Kadiri ya Mtakatifu Paulo Mungu hamwesabii mtu makosa yake bali amwomba achuchumalie upatanisho naye. Kumbe, jambo lililo la msingi ni toba. Kwa hakika Injili hii inazidi kukazia mafundisho ya Bwana tuliyoyasikia katika Injili ya Dominika iliyopita. Bwana anakutana na Mafarisayo na Waandishi wanaonung’unika kwa sababu eti yeye hula na watoza ushuru na wenye dhambi.

Mpendwa mwana wa Mungu mara moja Bwana anapohojiwa juu ya matendo yake ya upendo kwa walio wadhambi na watoza ushuru anaaanza mafundisho yake kwa kutoa mfano wa mwana mpotevu. Lengo la mfano huu ni kutaka kuonesha huruma ya Mungu isiyo na upeo, yaani inavuka uelewa na maarifa ya mwanadamu.

Katika mantiki ya kawaida mtu akipoteza mali ya urithi aliopewa na baba yake, basi inakuwa ndiyo mwisho wa kuwa na urithi, lakini katika Injili, Kristo anafundisha tofauti, yakwamba mmoja aliyeshupaa katika dhambi anaweza kusamehewa na Mungu cha msingi ni kusema “nitaondoka nitakwenda kwa Baba yangu na kumwambia, Baba nimekosa juu ya mbingu na mbele yako”. Na kisha Baba akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni akambusu sana”

Mpendwa mwana wa Mungu oneni jinsi upendo na huruma ya Mungu inavyovuta, huyu mtoto aliyekuwa amejiimarisha katika kiburi na ujeuri akishikilia dhana ya uhuru binafsi, anabadilika na kurudi katika njia ya toba na kumwelekea Baba yake. Oneni upendo wa Baba ulivyo na uvumilivu kiasi cha kukumbatia mtoto ambaye ananuka na harufu yake inatisha! Labda kwangu ingekuwa ngumu kukubaliana na harufu hii, lakini Mungu anatutaka tukatende kama yeye!

Mtoto aliyeona ananyanyaswa na hivi anaondoka nyumbani na sasa anarudi kwa unyenyekevu. Kipi chamfanya aondokane na kiburi hiki? Ni Neema ya Mungu. Habaki katika kiburi kama Mafarisayo na Waandishi wa sheria wanaoshikilia sheria na hivi kukataa kukiri dhambi zao. Tuna uhakika na tunasema ni Mungu anayetupatanisha naye, na kwa jinsi hiyo kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi.

Mpendwa msikilizaji, kuna jambo jingine la maana sana, yaani lile la Baba kutouliza ulikuwa wapi, na kwa nini ulitumia vibaya mali yako? Kwake yeye yatosha kusema nimekosa kama mfalme Daudi alivyomwambia Mungu nimekosa na mara moja akaambiwa hutakufa! Katika Injili ya leo Baba pasipo kuuliza kitu anamwandalia sherehe ya nguvu mwanae aliyeonekana.

Mpendwa wapo waamini ambao wamekuwa legelege kwa muda mrefu na kwa namna hiyo kufikiri wakati watakapoomba msamaha wataadhibiwa vikali, na hili uwafanya hata wabaki katika uvivu huo!

Mpendwa, Mungu haadhibu bali hukumbatia na kukufanyia sherehe ya furaha! Katika upendo huu wa Mungu wapo ambao hujiuliza, je kama Mungu awapenda wadhambi katika shida yao hiyo, inahaja gani kubadilika? Katika hili yatupasa kukumbuka Mungu ni upendo, uvumilivu na haki, lakini zawadi hii inadumu mpaka wakati wa kifo. Kama mpaka hapo mmoja amejiimarisha na kukomaa katika dhambi zake basi amejihukumu mwenyewe.

Katika mfano huu alioutoa Bwana, mwinjili atuonesha kwa njia ya mtoto mkubwa, aliyekuwa mwema jinsi mwanadamu anavyoweza kuingiliwa na wivu dhidi ya mdhambi anayetubu. Badala ya kufurahi kwa kuwa mdogo wake amerudi nyumbani yaani ametubu dhambi zake anachukia! Alisahau kwamba wema wake alionao ni zawadi toka kwa Mungu. Alisahau kuwa Jumuiya ya Kanisa ni jumuiya iliyo na wakosaji lakini pia iliyo safarini kuelekea ukamilifu toka dimbwi la dhambi. Tuwe basi makini tusije tukaanguka katika dhambi hiyo! Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.