2013-03-08 09:29:16

Domus Santae Mariae mahali watakapoishi Makardinali wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya!


Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako mwaka 1996 aliamua kufanya ukarabati mkubwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha ambayo kwa sasa inajulikana kama "Domus Santae Marthae" iliyoko ndani kabisa ya Mji wa Vatican. Hili ni jengo lenye ghorofa tano na lina vyumba 106 kwa ajili ya wageni maalum pamoja na vyumba 22 kwa matumizi ya mtu binafsi.

Uongozi wa Hosteli hii unateuliwa na Katibu mkuu wa Vatican kwa kuzingatia sheria na kanuni za Vatican. Kwa maneno mengine, huu ni Mfuko wa Mtakatifu Martha kama ulivyonuiwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili.

Hapa ni mahali panapotoa hifadhi na makazi kwa Makardinali, baadhi ya viongozi wanaofika mjini Vatican kwa shughuli za kiofisi. Katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa Papa Mpya, wale wote waliokuwa wanaishi kwenye Hosteli hii wameondolewa ili kutoa nafasi kwa Makardinali watakaoshiriki katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baadhi ya viongozi watakaoruhusiwa kuishi katika Hosteli hii ni wale waliotajwa kwenye Waraka wa Kichungaji kuhusu uchaguzi wa Papa, unaojulikana kwa lugha ya Kilatini kama " Universi Dominici Gregis".

Jengo hili lilijengwa na Papa Leo wa XIII kunako mwaka 1891, mwaka ambao unakumbukwa kutoka na kuzuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu kuzunguka viunga vya Mji wa Vatican na hivyo kupelekea watu wengi kupoteza maisha yao. Wakati wa Vita kuu ya Pili wa Dunia, Jengo hili lilitumika kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi, Wayahudi na Mabalozi wa Vatican kutoka katika nchi ambazo zilikuwa zimevunja uhusiano wa kidiplomasia na Italia.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipokuwa anafungua Mfuko huu alibainisha wazi kwamba, lengo ni kutoa huduma ya ukarimu kwa wageni wanaotembelea mjini Vatican, ili waweze kuonja ule upendo na mshikamano wa kidugu unaopaswa kujionesha miongoni mwa Makleri wanaotoa huduma yao kwenye Sekretarieti ya Vatican, wafanyakazi katika Mabaraza ya Kipapa, Makardinali na Maaskofu wanaofanya hija zao za kitume ili kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baadaye, iliamriwa kwamba, Jengo hili wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, litatumiwa na Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura na wale wote waliotajwa katika sheria kwenye mchakato huu. Viongozi hawa ni Katibu mkuu wa Makardinali, Mshehereshaji mkuu wa Liturujia za Kipapa, Mapadre walioteuliwa kwa ajili ya kutoa Sakramenti ya Upatanisho katika lugha mbali mbali.

Madaktari wawili kwa ajili ya kushugulikia dharura inapotokea. Wapishi na wafanyakazi wa ndani. Wote hawa hawana budi kuthibitishwa na Kardinali Camerlengo ambaye ndiye mratibu mkuu wa shughuli za Kanisa wakati ambapo kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro, kiko wazi. Wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, Makardinali wanaweza kutembea kwa miguu kutoka katika Jengo hili kuelekea kwenye Kikanisa cha Sistina, lakini pia kuna Bus maalum kwa ajili yao!








All the contents on this site are copyrighted ©.