Makardinali wanaoendelea na mchakato wa kumchagua Papa Mpya baada ya mkutano wao Jumatano,
tarehe 6 Machi 2013, jioni walikusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali
kwa ajili ya kuliombea Kanisa. Kwa namna ya pekee, wakati huu Makardinali wanajiaminisha
mikononi mwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa kwa kusali na kutafakari Rozari
Takatifu, muhtasari wa maisha na utume wa Yesu. Makardinali pamoja na waamini wanaokusanyika
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wanasali kwa lugha ya Kiitalia na Kilatini.
Baada
ya Rozari Takatifu, Makardinali walipata fursa ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kusali
katika ukimya, kama njia ya kuzungumza na Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu
na baadaye, walisali Masifu ya Jioni na Baraka ya Ekaristi Takatifu. Ibada hii imeongozwa
na Kardinali Angelo Comastri, Kasisi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Huu ndio utaratibu utakaofuatwa wakati huu Makardinali wanapoelekea kumchagua Khalifa
wa Mtakatifu Petro.